Featured Kitaifa

DC ILEJE AIPA KONGOLE EWURA KWA KUELIMISHA WADAU WA MAFUTA NA GESI

Written by mzalendoeditor

 

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) leo, tarehe 12 Julai 2025 imeendesha semina ya kuwajengea uelewa wadau wa mafuta na gesi ya kupikia katika Wilaya ya Ileje, mkoani Songwe. Semina hiyo iliyohusisha wajumbe wa Baraza la Biashara la Wilaya, watoa huduma wa bidhaa za mafuta na gesi na wafanyabiashara, imelenga kuhamasisha uwekezaji salama na endelevu katika sekta hiyo.

Akifungua semina hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Mhe. Farida Mgomi ameipongeza EWURA kwa kazi kubwa ya kuelimisha umma na kuitikia wito wa wilaya kuja kutoa mafunzo hayo muhimu.

“Nawapongeza sana EWURA kwa kazi nzuri wanayoifanya. Kuja kwenu Ileje ni hatua kubwa ya maendeleo kwa wananchi wetu. Mafunzo haya yataongeza uelewa kwa wawekezaji wetu wa ndani, kusaidia kupanua biashara zao kwa kufuata sheria na taratibu sahihi, na pia kuhakikisha usalama wa wananchi katika matumizi ya gesi na mafuta,” alisema Mhe. Mgomi.

Aidha, Mhe. Mgomi alieleza kuwa kupitia elimu hiyo, fursa zaidi za uwekezaji zitafunguka, huku akiahidi kuwa ofisi yake itaendelea kushirikiana na EWURA na wadau wengine katika kuboresha mazingira ya biashara wilayani humo.

Semina hii ni sehemu ya mwendelezo wa jitihada za EWURA katika kutoa elimu kwa umma na kuimarisha uelewa wa jamii kuhusu huduma za nishati.

About the author

mzalendoeditor