Wizara ya Katiba na Sheria imeendelea kutoa huduma za msaada wa Kisheria, Elimu ya Haki Uraia na Utawala Bora katika maonyesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea katika viwanja vya Sabasaba jijini Dar es Salaam ambapo wananchi wameendelea kupata haki zao zilizopotea.
Kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, Wizara imefanikiwa kurejesha tabasamu kwa Bi. Johari Ally ambaye alikua amenyang’anywa mtoto wake wa miaka miwili na Ndugu wa Baba aliyezaa naye.
Julai 10,2025 Bi Johari alifika katika banda la Wizara ya Katiba na Sheria akiwa anahitaji msaada wa kisheria wa namna ya kumpata mwanae aliyechukuliwa na ndugu wa baba yake kwa takribani miezi sita.
Baada ya kusikilizwa, wataalam wa Wizara waliweza kuwakutanisha mama wa mtoto na ndugu wa baba waliokuwa na mtoto ambapo walifanikiwa kumrejesha mtoto kwa mama yake na kuwashauri endapo watamuhitaji kwa ajili ya salaam wakubaliane na mama wa mtoto huyo.
Akizungumza baada ya kufanikiwa kumrejesha mtoto kwa mama yake, Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Haki za Binadamu, Bi. Beatrice Mpembo alisema kuwa haikua rahisi, changamoto zilikuwepo lakini kwa kuzingatia sheria za nchi zinamtaka mtoto wa umri huo akae na mama wao kama wataalam waliweza kushauri na kulifanikisha jambo hilo kwa amani.
Kwa upande wake Bi. Johari alitoa shukrani zake za dhati kwa Serikali na Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuendesha Kampeni ya Msaada wa Kisheria iliyomsaidia kumrejesha mwanae kwake.
Wizara ya Katiba na Sheria ipo katika viwanja vya Sabasaba ikiendelea kutoa huduma za msaada wa kisheria pamoja na elimu ya sheria na baada ya muda wa maonyesho kuisha wananchi wote wenye changamoto wanaweza kuwasiliana na Wizara ya Katiba na Sheria kupitia kituo cha Huduma kwa Mteja kwa namba 0262160360 kuanzia saa 1:30 asubuhi hadi saa 11:00 jioni.