Featured Kitaifa

SERIKALI LINDENI AMANI UCHAGUZI MKUU 2025 – JMAT

Written by mzalendoeditor

Katika kilele cha maandalizi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) imeitaka serikali kuhakikisha kuwa amani ya taifa inadumishwa na kulindwa kwa nguvu zote dhidi ya vitendo vyovyote vinavyoashiria kuvunjika kwa tunu hiyo ya kitaifa.

Akizungumza leo Julai 8,2025 katika mkutano mkuu wa JMAT uliofanyika jijini Dodoma, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Dkt. Alhad Mussa Salum, amesema kuwa lengo kuu la kuanzishwa kwa jumuiya hiyo ni kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kudumisha na kuilinda amani, hasa katika vipindi vya siasa ambapo joto la uchaguzi huwa juu.

“Tanzania imejengwa juu ya msingi wa amani, na ni wajibu wetu sote, serikali, taasisi za kiraia, viongozi wa dini, na wananchi kwa ujumla kuitunza. Hatuwezi kuruhusu chuki, migawanyiko au lugha za uchochezi kuharibu misingi hii imara,” amesema Dkt. Salum.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa JMAT, Dkt. Israel Maasa Ole Gabriel, amesema jumuiya hiyo imejipanga kuimarika zaidi kitaasisi kwa kujenga makao makuu na kumbi za mikutano jijini Dodoma. Hata hivyo, aliiomba serikali kusaidia kwa kutoa eneo la ardhi litakalowezesha utekelezaji wa mpango huo.

“Tuna ndoto ya kuwa na kituo cha kitaifa cha amani mahali ambapo watu kutoka pande zote za nchi wataweza kujifunza, kujadiliana, na kutafuta suluhu ya changamoto za kijamii na kisiasa kwa njia ya mazungumzo,” amesema Dkt. Ole Gabriel.

Mkutano huo pia ulihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ambaye pia ni mlezi wa JMAT katika mkoa huo, Mhe. Rosemary Senyamule. Akiwahutubia wajumbe wa mkutano huo, Mhe. Senyamule aliwataka kuwa mabalozi wa maridhiano na kuhamasisha wananchi kuwa mstari wa mbele kulinda amani ya nchi.

“Amani ni msingi wa maendeleo na ustawi wa jamii yoyote. Nawasihi msiishie kwenye mikutano pekee, bali mfike kwa jamii na mtoe elimu kuhusu namna bora ya kushiriki uchaguzi kwa njia ya amani na maridhiano,”amesema Mhe. Senyamule.

Mkutano huo umeleta pamoja viongozi wa dini, wawakilishi wa mashirika ya kiraia, na wadau wa amani kutoka mikoa mbalimbali, na unatarajiwa kuwa chachu ya mikakati mipya ya kudumisha mshikamano wa kitaifa kuelekea uchaguzi mkuu.

About the author

mzalendoeditor