Featured Kitaifa

MKURUGENZI MTENDAJI WA STAMICO AIPONGEZA TUME YA MADINI KWA KUVUKA MALENGO YA MAKUSANYO KWA MWAKA 2024/2025

Written by mzalendo

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Dkt. Venance Mwasse, ameipongeza Tume ya Madini kwa mafanikio makubwa ya kuvuka lengo la makusanyo ya mapato kwa mwaka wa fedha 2024/2025, ambapo imekusanya kiasi cha shilingi trilioni 1.071 dhidi ya lengo la shilingi trilioni 1.

Akizungumza wakati wa ziara yake katika banda la Tume ya Madini kwenye Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba), yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu J.K. Nyerere, Dar es Salaam, Dkt. Mwasse amesema mafanikio hayo ni matokeo ya usimamizi makini, matumizi ya teknolojia, na ubunifu unaoendelea ndani ya Tume.

“Mafanikio haya ni uthibitisho kuwa sekta ya madini ni nguzo imara ya uchumi wa nchi. Kama alivyosema Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, madini siyo nyanya tuziache zioze – yanapaswa kuchimbwa kwa weledi na kwa kutumia wataalamu wa ndani. Tume ya Madini imetekeleza hilo kwa vitendo,” amesisitiza Dkt. Mwasse.

Aidha, ameeleza kuwa utekelezaji wa mabadiliko ya sheria ya madini umechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio haya, hususan kupitia sera ya Ushiriki wa Watanzania katika Sekta ya Madini (Local Content), inayotoa fursa kwa wazawa kushiriki kikamilifu katika huduma, ajira na biashara zinazohusiana na sekta ya madini.

Amebainisha kuwa STAMICO ni miongoni mwa mashirika yaliyonufaika moja kwa moja na utekelezaji wa sera hiyo.

Kwa upande wake, Afisa Sheria Mwandamizi kutoka Tume ya Madini, Bw. Damian Kaseko, ameeleza kuwa Tume ilianzishwa rasmi mwaka 2017 chini ya Sheria ya Madini Na. 7, ikiwa na jukumu la kusimamia kikamilifu shughuli zote za madini nchini. Tangu kuanzishwa kwake, Tume imeendelea kuimarika na kuwa chombo madhubuti katika kusimamia rasilimali za madini kwa manufaa ya Taifa.

Makusanyo haya ya kihistoria ni kielelezo cha mafanikio ya kimkakati katika sekta ya madini na mchango wake mkubwa katika kukuza uchumi wa Taifa, huku yakionesha uwezekano mkubwa wa sekta hiyo kuwa chachu ya maendeleo endelevu kwa Watanzania wote.

About the author

mzalendo