Featured Kitaifa

MFUMO WA STAKABADHI ZA GHALA KUIBADILISHA TASWIRA YA BIASHARA YA MAZAO TANZANIA

Written by mzalendoeditor

Na Alex Sonna,Dar es Salaam

Katika jitihada za kuimarisha soko la mazao na kuinua kipato cha wakulima, Bodi ya Usimamizi wa Mfumo wa Stakabadhi za Ghala (WSRB) imejipanga kuhakikisha mfumo huo unafahamika kwa wananchi wengi zaidi, hususan wazalishaji na wadau wa kilimo nchini.

Kupitia ushiriki wake katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba, Bodi hiyo inaendelea kutoa elimu ya kina kuhusu namna mfumo huu unavyoweza kuwa mkombozi wa kweli kwa wakulima wa Tanzania.

Akizungumza katika maonesho hayo, Afisa Mipango wa Bodi hiyo, Baraka Ndabila, amesema mfumo huu pia unawawezesha wakulima kupata mikopo kupitia stakabadhi walizopewa, hali inayowaongezea uwezo wa kifedha na kupanua shughuli zao za kilimo.

“Kwa kutumia stakabadhi kama dhamana, mkulima anapata nafasi ya kupumua kiuchumi huku akiendelea kusubiri muda muafaka wa kuuza mazao yake,” amefafanua.

Ameeleza kuwa kwa miaka mingi, wakulima wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya kuuza mazao yao kwa bei duni mara baada ya mavuno kutokana na kukosa uwezo wa kuyahifadhi hadi bei ya soko itakapopanda.

Amesema Mfumo wa stakabadhi za ghala unalenga kubadilisha hali hii kwa kuwezesha wakulima kuhifadhi mazao yao kwenye maghala yaliyosajiliwa, kupata stakabadhi rasmi na kuuza mazao hayo kwa wakati wa bei nzuri.

“Elimu inayotolewa inahusu taratibu za usajili wa maghala, masharti ya kuhifadhi mazao, mchakato wa kupata stakabadhi, pamoja na haki na wajibu wa pande zote zinazohusika,lengo ni kuhakikisha kuwa mfumo huu unafanyika kwa uwazi, usalama na ufanisi wa hali ya juu, “ameeleza

Ndabila amebainisha kuwa moja ya malengo ya msingi ya Bodi ni kuhakikisha maghala yanayosajiliwa yanakidhi vigezo vya kitaifa na kimataifa, ikiwa ni pamoja na ubora wa miundombinu, usalama wa mazao, na uwazi wa taarifa kwa wateja.

“Hii ni muhimu ili kujenga imani kwa wakulima na taasisi za kifedha zinazotoa mikopo kwa kutumia stakabadhi hizo,takwimu zilizopo, maeneo mengi ya kilimo nchini bado hayajanufaika kikamilifu na mfumo huu kutokana na uelewa mdogo,ndiyo maana Bodi imeamua kuutumia mwamko wa watu katika maonesho ya Sabasaba kama jukwaa la kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa wakati mmoja, “amefafanua

Licha ya hayo ameeleza kuwa Bodi pia imekuwa ikihamasisha ushiriki wa sekta binafsi katika uendeshaji wa maghala, jambo linalotarajiwa kuongeza ushindani wa kutoa huduma bora na kuongeza idadi ya maghala yaliyosajiliwa nchini.

Aidha, baadhi ya wakulima waliotembelea banda la Bodi hiyo katika maonesho hayo wameelezea kufurahishwa na elimu waliyoipata na kuonyesha nia ya kuanza kutumia mfumo huo ili kuondokana na changamoto walizokuwa wakikumbana nazo awali.

Wameeleza kuwa kupitia elimu hiyo wanayoipata watarajia kuongezeka kipato pamoja na ukuaji wa sekta ya kilimo kwa ujumla .

About the author

mzalendoeditor