Watumishi wa Jeshi la Magereza wameipongeza na kuishukuru Serikali kwa kuwapatia majiko ya gesi ya Kilogramu 15 pamoja na majiko ya sahani mbili huku wakiahidi kuwa mabalozi wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Wakizungumza leo Julai 04, 2025 wakati wa hafla fupi ya kupokea mitungi hiyo ya gesi pamoja na majiko ya sahani mbili kutoka kwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Askari pamoja na Maafisa wa Jeshi hilo wamesema kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia itawaongezea ufanisi katika majukumu yao.
“Kwanza tungependa kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kinara katika kuhakikisha Watanzania tunaachana na matumizi ya nishati zisizo safi na salama za kupikia.
Kwetu sisi Jeshi la Magereza ameweza kutoa fedha zilizowezesha kufungiwa mifumo ya nishati safi ya kupikia magerezani. Matumizi ya kuni katika Magereza yetu yamekuwa ni historia. Pamoja na jitihada hizo na sasa katukumbuka Watumishi wa Jeshi la Magereza, kwa kweli tunamshukuru sana na tunampongeza sana,” amesema Mkuu wa Magereza Mkoa wa Geita, ACP. Jonam Mwakasagule.
Kwa upande wake Mkaguzi Msaidizi Jackline Kasansa ameshukuru kwa elimu kuhusu nishati safi waliyopata na kuahidi kuwa watakwenda kuwa mabalozi wa nishati safi ya kupikia kwa jamii inayowazunguka.
“Mimi kama mama na kama mtumishi, kuna muda nachelewa kurudi kutokana na majukumu yetu lakini kwa sasa hata nikichelewa kurudi naweza kuandaa chakula kwa ajili ya familia yangu kwa haraka zaidi tofauti na hapo awali. Kwa kweli nina furaha sana. Namshukuru sana Mhe. Rais pamoja na wote waliowezesha hili kufanikiwa,” amesema Koplo Leonida.
Awali akizungumza kabla ya ugawaji wa majiko hayo kwa watumishi wa jeshi hilo Mkoa wa Geita, Mjumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Lucas Malunde amesema kuwa ugawaji wa mitungi hiyo ya gesi pamoja na majiko yake ni muendelezo wa jitihada za serikali katika kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ambao umebainisha kuwa kufikia mwaka 2034, asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia.
“Tangu kuzinduliwa kwa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia, REA tumeendelea kuwezesha, kuhamasisha na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa nishati safi ya kupikia. Kila mmoja akawe balozi wa kuendelea kutoa elimu na kuhamasisha wengine kutumia nishati safi ya kupikia. Kwa pamoja tutaweza kufikia malengo pamoja na kuokoa mazingira,” amebainisha Malunde.
Kaimu Meneja Usaidizi wa Kiufundi kwa Wawekezaji Miradi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Emmanuel Yesaya amesema kuwa jumla ya mitungi ya gesi ya Kilogramu 15 na majiko ya gesi ya sahani mbili 310 itagaiwa bure kwa Watumishi wa Magereza Mkoa wa Geita.