Mjumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Lucas Malunde (katikati) akimkabidhi Askari wa Jeshi la Magereza jiko la gesi la sahani mbili wakati wa hafla ya ugawaji wa mitungi ya gesi ya Kilogramu 15 pamoja na majiko ya sahani mbili kwa Watumishi 557 wa Jeshi hilo Mkoa wa Mwanza iliyofanyika jana Julai 03, 2025 katika Gereza la Butimba, Mwanza. Kulia ni Kaimu Meneja Usaidizi wa Kiufundi kwa Wawekezaji Miradi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Emmanuel Yesaya.
Mjumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Lucas Malunde (katikati) akiwa kwenye picha moja na Maafisa pamoja na Askari wa Jeshi la Magereza Mkoa wa Mwanza mara baada ya hafla ya ugawaji wa mitungi ya gesi ya Kilogramu 15 pamoja na majiko ya sahani mbili kwa Watumishi 557 wa Jeshi hilo Mkoa wa Mwanza iliyofanyika jana Julai 03, 2025 katika Gereza la Butimba, Mwanza.
Mjumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Lucas Malunde (katikati) akimkabidhi Askari wa Jeshi la Magereza jiko la gesi la sahani mbili wakati wa hafla ya ugawaji wa mitungi ya gesi ya Kilogramu 15 pamoja na majiko ya sahani mbili kwa Watumishi 557 wa Jeshi hilo Mkoa wa Mwanza iliyofanyika jana Julai 03, 2025 katika Gereza la Butimba, Mwanza. Kulia ni Kaimu Meneja Usaidizi wa Kiufundi kwa Wawekezaji Miradi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Emmanuel Yesaya.
…….
Watanzania wameendelea kuhamasishwa kutumia nishati safi ya kupikia ili kulinda mazingira kwa vizazi vijavyo.
Wito huo umetolewa leo Julai 03, 2025 na Mjumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Lucas Malunde wakati wa hafla ya ugawaji wa mitungi ya gesi ya Kilogramu 15 pamoja na majiko ya sahani mbili kwa Watumishi 557 wa Jeshi la Magereza Mkoa wa Mwanza iliyofanyika katika Gereza la Butimba.
“Matumizi ya nishati safi ya kupikia licha ya kuokoa vifo vitokanavyo na matumizi ya nishati zisizo safi na salama, lakini pia inatusaidia kutunza mazingira. Tumerithishwa nchi hii ikiwa na uoto wa asili mzuri, miti na hewa safi, hivyo basi hatuna budi na sisi kufanya jitihada zote kuhakikisha tunarithisha kizazi kijacho mazingira safi pamoja na hewa safi.
Na yote hayo yanawezekana kwa kila mmoja kuunga mkono Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia pamoja na kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye anatamani kuona kila mwananchi akitumia nishati safi ya kupikia,” amesema Mjumbe huyo Malunde.
Ameongeza kuwa, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inatekeleza miradi mbalimbali ya kuhakikisha wananchi wanaachana na matumizi ya nishati zisizo safi na salama za kupikia.
Amebainisha kuwa moja ya mradi wa unaotekelezwa na REA kwa ajili ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ni ujenzi wa mifumo ya nishati safi ya kupikia katika Magereza zote nchini ambazo sasa zinatumia nishati safi ya kupikia.
“Mhe. Rais kama kinara wa nishati safi ya kupikia akaona pia atoe fedha kwa ajili ya kuwezesha na watumishi wote wa Jeshi la Magereza nchini kupata mitungi ya gesi ya kupikia ya Kilogramu 15 pamoja na majiko yake ya sahani mbili. Mkawe mabalozi wazuri wa nishati safi ya kupikia ili lengo la Serikali la kuhakikisha ifikapo 2034, asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia,” amesema.
Awali akitoa taarifa kuhusu mradi huo, Kaimu Meneja Usaidizi wa Kiufundi kwa Wawekezaji Miradi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Emmanuel Yesaya ametoa rai kwa watumishi wa jeshi la magereza wote nchini kutunza miundombinu ya nishati safi ya kupikia iliyofungwa katika magereza kwa kuwa serikali imetumia gharama kubwa kuweka miundombinu hiyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Magereza Mkoa wa Mwanza, SACP. Masudi Kimolo ameishukuru Serikali kupitia REA kwa kuweza kuwafikishia nishati hiyo watumishi wa Jeshi la Magereza katika Mkoa wa Mwanza na kusema kuwa mitungi hiyo ya gesi iliyogaiwa bure imekuwa ni motisha kwa watumishi hao na kuahidi kuwa mabalozi wa nishati safi ya kupikia kwa jamii inayowazunguka.
Wakala wa Nishati Vijijini uliingia makubaliano na Jeshi la Magereza Septemba 13, 2024 uliolenga kuwezesha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa Magereza yote nchini.
Mkataba huo wenye gharama ya Shilingi Bilioni 35.23 umelenga kuwezesha ujenzi wa miundombinu ya gesi asilia, ujenzi wa miundombinu ya biogas, ujenzi wa miundombinu LPG, usambazaji wa mitungi ya gesi pamoja na majiko ya sahani mbili kwa watumishi wa magereza, usambazaji wa mkaa mbadala, ununuzi wa mashine za kutengenezea mkaa mbadala na kuwajengea uwezo watumishi wa magereza kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia.