Naibu Waziri wa Wizara ya Katiba na Sheria Mhe. Jumanne Sagini amewataka Waajiriwa wapya wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwenda kuitumia vizuri nafasi waliyopata katika Utumishi wa Umma kwa kuitumikia Serikali kwa weledi na kutenda haki kwa wananchi wanaokwenda kuwahudumia.
Naibu Waziri amebainisha hayo wakati akifungua Mafunzo elekezi ya awali kwa Waajiriwa Wapya wa Ofisi yaTaifa ya Mashtaka (Orientation and Basic Induction Course) yaliyoandaliwa na Ofisi hiyo kwa kushirikiana na Chuo cha Utumishi wa Umma yanayofanyika tarehe 01 hadi 04 Julai, 2025 Mkoani Iringa.
Mafunzo hayo yamejumuisha jumla ya washiriki 148 ambapo kuna Makatibu Sheria 20, Mawakili wa Serikali 102, Madereva 24, Muhasibu 01 na Msaidizi wa Maktaba 01.
Katika hotuba yake Mhe. Sagini amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kibali cha Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kuajiri watumishi wanaowahitaji ili kutekeleza majukumu yake.
“Kuanzisha ofisi bila watumishi wa kutosha kunasababisha mashauri kutokuisha kwa wakati, haki za watu kuchelewa na kupindishwa.” Amesema Mhe. Sagini.
Amesema Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ni muhimili muhimu wa utekelezaji wa haki na ulinzi wa maslahi ya umma kupitia mashauri ya jinai kwa maana hiyo waliopata nafasi ya kuajiriwa katika ofisi hiyo wamepewa dhamana kubwa ya kuitumikia Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uaminifu, weledi na uzalendo.
Kadhalika ameongeza kuwa Mafunzo hayo yameandaliwa kwa lengo la kuwajengea uelewa mpana wa majukumu yao, miiko ya kazi, misingi ya sheria pamoja na utamaduni wa utumishi wa umma, pia ni fursa ya kujenga mshikamano baina yao ili kuwawezesha kufanya kazi kwa ushirikiano bila kujali tofauti za kada, maeneo wanayotokea na imani zao.
‘’ Muwe waadilifu katika kuwahudumia wananchi pamoja na kuzingatia, Kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali ya serikali, tunahitaji watumishi, wachapakazi, wanaozingatia sheria, taratibu na miongozo ya kazi na wanaojivunia kufanya kazi kwa uaminifu.” Amesema Naibu Waziri.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Sylvester Mwakitalu ameushukuru Uongozi wa Wizara ya Katiba na Sheria kwa mchango wao mkubwa walioutoa hadi kufikia hatua ya Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kupata kibali cha kuajiri watumishi wapya mfululizo.
Amesema Wizara imeendelea kuwashika mkono na kuwawezesha kupata vitendea kazi pamoja na kuwawezesha kufungua ofisi katika wilaya 108 na zimebaki jumla ya wilaya 31 ambazo baadhi zinatarajiwa kufunguliwa ndani ya mwaka wa fedha ulioanza 2025/2026.
Mkurugenzi Mwakitalu amefafanua kuwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka imekabidhiwa majukumu nyeti ambayo yanagusa haki za watu, kwa sababu ya unyeti wa majukumu hayo waliona hawawezi kuruhusu kundi hili la watumishi wapya waende kutekeleza majukumu kabla hawajapata mafunzo ili waweze kuzijua kanuni, taratibu, Sheria na sera zinazoongoza utumishi wa umma.
Sambamba na hilo ameeleza lengo la mafunzo hayo ni kuwaandaa Waajiriwa wapya kuingia katika Utumishi wa Umma wakiwa wanajua nini maana ya Utumishi wa Umma na wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi iliyowekwa ya utumishi wa umma.
“Ofisi ya Taifa ya Mashtaka ni timu moja na lengo letu ni kutoa huduma bora za mashtaka kwa wote, kwa wakati, kwa haki na kwa usawa.” Amesema Mkurugenzi wa Mashtaka.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Iringa Bw. Benjamin Sitta amewaasa Waajiriwa Wapya kwenda kufanya kazi kwa kuzingatia haki za wananchi kwani pasipo na haki hakuna amani, haki ikishatoweka amani itakuwa ni shida kupatikana.