Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mha. Hamad Yussuf Masauni akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam Juni 30, 2025 mara baada ya kupokea Taarifa ya Tathmini ya Mwenendo wa Biashara ya Kaboni kutoka kwa Kamati ya Biashara ya kaboni.
PICHA NA OFISI YA MAKAMU WA RAIS
Mwandishi Wetu -Dar es Salaam
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mha. Hamad Yussuf Masauni amesema Biashara ya Kaboni ni miongoni mwa nyenzo muhimu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambapo nchi, taasisi, kampuni na wananchi wanaweza kushiriki katika jitihada za Kitaifa na Kimataifa za kupunguza gesijoto duniani.
Waziri Masauni amesema hayo jijini Dar es Salaam Juni 30, 2025 mara baada ya kupokea Taarifa ya Tathmini ya Mwenendo wa Biashara ya Kaboni kutoka kwa Kamati ambapo amesema Tanzania imeimarisha usimamizi wake kwa kuanzisha Kanuni za mwaka 2022 na marekebisho yake ya mwaka 2023, pamoja na Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni (NCMC).
Amesema NCMC ina jukumu la kusajili miradi, kuwezesha ufuatiliaji, uthibitishaji wa gesijoto, utoaji wa elimu na uhamasishaji wa wadau. Tangu kuanza kutumika kwa kanuni, jumla ya miradi 73 ambayo miradi 69 ipo katika hatua mbalimbali za usajili na miradi 4 ipo katika hatua ya utekelezaji.
Ameongeza kwa upande wa Zanzibar imeanza kupokea maombi ya miradi ya kaboni kufuatia kupitishwa kwa Kanuni za Udhibiti na Usimamizi wa Biashara ya Kaboni za mwaka 2025. Kufikia Mei 2025, kampuni nne (4) zilionesha nia ya kutekeleza miradi hiyo, ambapo mbili (2) kati yao zimewasilisha maandiko dhana.
“Kamati hii ilipewa jukumu la kufanya tathmini na kutoa mapendekezo ya kuongeza ufanisi wa uendeshaji wa biashara ya Kaboni nchini, lengo kuu ni kufanya tathmini ya hali ya sasa ya biashara ya kaboni nchini Tanzania na kutoa mapendekezo kwa serikali kuhusu njia bora za kuimarisha mifumo na mwenendo wa biashara ya kaboni Tanzania Bara na Zanzibar.
Amesema katika kuimarisha uelewa na ushirikishwaji wa wadau katika Biashara ya Kaboni, Serikali kwa kushirikiana na wadau imeendelea kutoa elimu kwa Umma ili kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu biiashara hiyo.
Amesema Kamati imependekezwa kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu Biashara ya Kaboni, kuandaa miongozo ya mafunzo kwa wadau wa ngazi zote, pamoja na kuanzishwa majukwaa ya wadau la majadiliano katika ngazi mbalimbali.
“Utekelezaji wa Biashara ya Kaboni nchini utaimarika kwa kufanya mapitio ya kanuni na miongozo ya biashara ya Kaboni, kuboresha rejesta ya Taifa ya Kaboni, kuweka mkakati mahususi wa utoaji wa elimu kwa umma, kuboresha mifumo ya usimamizi na utunzaji wa takwimu na kuhamasisha ushirikishwaji wa wadau ikiwemo sekta binafsi.
Ameongeza kwa upande wa Miradi ya kimkakati kunufaika na Biashara ya Kaboni, Tathmini inaonesha kuwa Tanzania ina nafasi kubwa ya kunufaika na Biashara ya Kaboni kupitia utekelezaji wa miradi ya kimkakati katika sekta mbalimbali, ikiwemo reli ya kisasa ya umeme (SGR), Mabasi yaendayo haraka (Dar es Salaam Rapid Transit – DART), uzalishaji wa umeme, gesi asilia, misitu, kilimo, majengo, elimu, madini, udhibiti wa taka na uchumi wa buluu.