Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango, leo tarehe 29 Juni 2025 amewasili nchini Hispania ambapo anatarajiwa kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Mkutano wa Nne wa Kimataifa wa Ufadhili wa Maendeleo (FfD4) utakaofanyika Jijini Sevilla kuanzia tarehe 30 Juni hadi 03 Julai 2025.
Mkutano huo unatoa fursa ya kipekee ya kuboresha ufadhili katika ngazi mbalimbali ikiwa ni pamoja na kusaidia mabadiliko ya muundo wa kifedha wa kimataifa na kushughulikia changamoto za ufadhili zinazozuia msukumo wa uwekezaji unaohitajika haraka kwa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).
Washiriki katika Mkutano huo ni pamoja na Viongozi Wakuu wa Nchi na Serikali, Mashirika ya Kikanda na Kimataifa, Taasisi za Kifedha, Wafanyabiashara na Asasi za Kiraia.
Aidha, Makamu wa Rais anatarajiwa kushiriki katika Mikutano ya Uwili yenye lengo la kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania, Mataifa na Taasisi zinazoshiriki mkutano huo.