Featured Michezo

MAVUNDE AONGOZA  WATUMISHI WA WIZARA YA MADINI KATIKA BONANZA LA KUIMARISHA AFYA NA MSHIKAMANO

Written by mzalendoeditor

Na Alex Sonna,Dodoma

Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, ameungana na watumishi wa Wizara ya Madini pamoja na taasisi zake kushiriki katika Bonanza la Michezo lililofanyika jijini Dodoma, likiwa na lengo la kuimarisha afya, mshikamano, na kuongeza morali ya utendaji kazi.

Akizungumza kwenye bonanza hilo leo June 28,2025 Mavunde amesema bonanza hilo linaendana na dhamira ya Serikali ya kuhakikisha watumishi wa umma wana afya bora, mazingira rafiki ya kazi na moyo wa kujituma.

Amesisitiza kuwa kauli mbiu ya “Madini ni Maisha na Utajiri” inapaswa kuakisiwa na namna watumishi wanavyojijenga kiafya na kifikra ili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

“Nimefurahi kuwa sehemu ya bonanza hili, ambalo si tu linajenga afya, bali linatuunganisha kama familia ya madini,tuendelee kuwa timu moja yenye malengo ya pamoja ili mchango wa sekta hii muhimu uendelee kuonekana,” amesema Mavunde.

Akimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Waziri huyo ameeleza kuwa mafanikio makubwa ya wizara hiyo yametokana na uongozi wake thabiti na uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya madini.

“Aidha,nampongeza Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini kwa kusimamia vema wafanyakazi na kuunda mazingira mazuri ya kazi yenye nidhamu na mshikamano,uongozi mzuri wa Katibu Mkuu umesaidia kujenga ari kazini, na leo tumeanza mwaka mwingine wa fedha tukiwa na malengo makubwa,naomba tuendelee kujituma kwa ajili ya mafanikio ya wizara na taifa,” ameongeza Mavunde.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba,amesema bonanza hilo ni sehemu ya mkakati wa menejimenti kuhakikisha watumishi wanabaki kuwa na afya njema, ikizingatia kuwa mazoezi ni kinga muhimu dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza.

“Tunaamini mtumishi mwenye afya ni mtendaji bora,bonanza hili ni la kufunga mwaka wa fedha, na tunatarajia kuendeleza utamaduni huu kwa kuzingatia umuhimu wa afya na mshikamano kazini,” amesema Katibu Mkuu.

Ametaja faida za Bonanza kwa Watumishi wa Wizara ya Madini,Kuimarisha afya na kuongeza kinga ya mwili,Kukuza mshikamano na mawasiliano kazini,Kuhamasisha nidhamu na morali ya utendaji na Kuongeza tija na ufanisi katika kutekeleza majukumu .

Aidha, amempongeza Waziri Mavunde kwa kuwa kiongozi wa karibu na mwenye kusikiliza wafanyakazi , hali inayowafanya watumishi kujivunia kuwa sehemu ya sekta ya madini.

Nao watumishi kwa pamoja wamempongeza Waziri huyo wa Madini kwa mafanikio ya uongozi wake, huku Kamishna wa Madini, Dkt. Abdulrahman Mwanga, akisema kuwa uwazi na mshikamano katika uongozi wa wizara hiyo umeongeza tija na hamasa ya kazi miongoni mwa watumishi.

Bonanza hilo lilihusisha michezo mbalimbali kama mpira wa miguu, kuvuta kamba, mbio na michezo ya kufurahisha, na limetajwa kuwa jukwaa muhimu la kujenga mahusiano chanya kazini na kuongeza ari ya kuwajibika kwa watumishi wa wizara hiyo.

About the author

mzalendoeditor