Featured Kitaifa

ZAIDI YA WASHIRIKI 250 KUTOKA NCHI MBALIMBALI KUSHIRIKI TUZO ZA UTALII DUNIANI 2025

Written by mzalendoeditor

Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk. Pindi Chana,akizungumza na wanandishi wa habari leo Juni 26,2025 jijini Dodoma  kuhusu utoaji tuzo za Utalii Duniani (World Travel Awards) kwa Kanda ya Afrika na Bahari ya Hindi zitakazofanyika Juni 28, 2025 jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk. Pindi Chana,akizungumza na wanandishi wa habari leo Juni 26,2025 jijini Dodoma  kuhusu utoaji tuzo za Utalii Duniani (World Travel Awards) kwa Kanda ya Afrika na Bahari ya Hindi zitakazofanyika Juni 28, 2025 jijini Dar es Salaam.

Na.Alex Sonna-DODOMA

 

TANZANIA imepewa heshima ya kuwa mwenyeji wa tukio la utoaji Tuzo za Utalii Duniani (World Travel Awards) kwa Kanda ya Afrika na Bahari ya Hindi kwa mwaka 2025 ambapo itashiriki katika kuwania vipengele 50.

Hayo yamesemwa leo Juni 26,2025 jijini Dodoma na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk. Pindi Chana,wakati akizungumza na wanandishi wa habari kuhusu utoaji tuzo hizo utakazofanyika Juni 28, 2025 jijini Dar es Salaam.

Amesema kwa mwaka huu 2025 tuzo zilizotangazwa kushindaniwa na WTA ni pamoja na Eneo bora kwa Utalii Afrika,  Bodi bora ya Utali, Kivutio Bora cha Utalii Afrika,  Hifadhi bora zaidi Afrika, Kampuni Bora za Utalii, Hoteli inayotoa Huduma Bora kwa Watalii pamoja na Kampuni Bora ya Huduma za Safari.

“Kama nchi  kwa ushirikiano baina ya Sekta za Umma na Binafsi tumeingia katika kinyang’anyiro hiki katika vipengele 50 kupitia vivutio, huduma bora pamoja na ukarimu wetu kwa watalii.”amesema Dkt.Chana

Aidha Dkt.Chana amesema kuwa  zaidi ya washiriki 250 kutoka nchi mbalimbali tayari wamethibitisha kushiriki, wakiwemo viongozi wa sekta ya utalii, wawekezaji, waandishi wa habari wa kimataifa na watoa huduma wa sekta hiyo kutoka Afrika na visiwa vya Bahari ya Hindi.

“Namshukuru Rais Samia kwa maono yake katika sekta hii ya utalii ikiwemo maelekezo hususan jitihada alizozifanya hususan kuimarisha uwekezaji katika Sekta ya utalii kupitia kampeni ya Tanzania, The Royal Tour, maboresho ya miundombinu, na sera zinazowezesha Sekta hii kukua kwa kasi.”amesema 

Dkt.Chana ametoa wito kwa Watanzania kujivunia nafasi hiyo ya kihistoria na kumshukuru Rais Samia kwa kuendeleza sera, miundombinu na uwekezaji unaoifanya Tanzania kuendelea kung’ara kimataifa kama kitovu cha utalii Afrika.

Tuzo hizo zilianzishwa mwaka 1993 nchini Uingereza na zimekuwa zikitolewa kwa mfululizo kwa miaka 32, zikilenga kutambua ubora katika huduma za utalii duniani. Tanzania ilianza kushiriki mwaka 2013 na imekuwa ikijizolea tuzo kila mwaka, ikiwemo ile ya Kivutio Bora kupitia Mlima Kilimanjaro.

About the author

mzalendoeditor