Featured Kitaifa

MAABARA YA MADINI TANZANIA NESCH MINTECH YAAMINIKA SAUDI ARABIA

Written by mzalendoeditor

Na Mwandishi Wetu

Kampuni ya New Future Mining (NFMC) imetangaza makubaliano ya kimkakati na Maabara ya madini ya Nesch Mintech Pvt Ltd ya jijini Mwanza kuanzisha kituo cha kisasa cha maabara NFMC LAB kwa huduma za Kisasa za Upimaji na Uchambuzi wa Madini jijini Jeddah, Saudi Arabia.

Mkurugenzi wa New Future Mining Company, Mohammed Alomoudi amesema NFMC LAB itaendeshwa na Nesch Mintech, ikitumia utaalamu uliothibitishwa kimataifa kwa kiwango cha ISO 17025:2017 na mbinu bora za maabara ili kuhakikisha huduma zenye viwango vya juu vya kimataifa kwa kampuni za uchimbaji na utafiti wa madini kote nchini na katika ukanda wa Mashariki ya Kati.

Bw. Alomoudi mesema, “Kwa kushirikiana na Nesch Mintech, tunapiga hatua muhimu katika kuleta maabara ya viwango vya kimataifa nchini Saudi Arabia. Ushirikiano huu unasaidia moja kwa moja malengo ya Dira ya Maendeleo ya Saudi Arabia ya 2030, kwa kulenga kuhamasisha uwekezaji wa kiteknolojia, kuendeleza ujuzi wa ndani, na kuleta uhamishaji wa maarifa kutoka kwa wataalamu wa kimataifa kwenda kwa mafundi na wakemia wa Kisaudi”.

Utiaji Saini huu uliofanyika jijini Dar es Salaam tarehe 26 Juni 2025 umeshuhudiwa na Mkurugenzi wa kituo cha uwekezaji Tanzania (TIC), Gelead Teri na Balozi wa Saudi Arabia nchini Tanzania Yahya Ahmed Okeish.

Naye Mkurugenzi wa kampuni ya Nesch Mintech Happiness Neganda Nesvinga amesema maabara hiyo itaendesha mafunzo ya kina kwa watendaji wa ndani ili kuhakikisha kizazi kipya cha wataalamu wa madini kilicho tayari kwa changamoto za kimataifa ikiwa ni hatua msingi Ya kuibuka kwa NFMC LAB kama kitovu cha kikanda cha ubora wa uchambuzi wa madini.

Naye Mkurugenzi wa kituo cha uwekezaji Tanzania (TIC), Bw. Gelead Teri ameipongeza Nesch Mintec kwa mafanikio haya, akisisitiza kuwa serikali inathamini na kuunga mkono wawekezaji wa ndani na kuongeza kuwa mafanikio ya kampuni hiyo katika masoko ya kimataifa ni ushahidi tosha kuwa watanzania wanaweza kushindana katika masoko ya dunia.

Ameongeza kuwa faida ya ushirikiano huu ni ⁠kuongeza ajira kwa Watanzania, ⁠kufanya Uhamisho wa kiteknolojia kwani nchi hizi mbili zitashirikiana teknolojia mbalimbali,⁠ ⁠kupandisha uchumi wa Tanzania,⁠ ⁠na Tanzania kuwa kitovu cha ubunifu wa kikanda kwa sekta ya madini

Nesch Mintech ni mtoa huduma wa kimataifa wa maabara za uchunguzi na upimaji wa madini imekuwa ikihudumu kwa fahari nchini Tanzania kwa zaidi ya miaka kumi, ikitoa huduma za kisasa za upimaji wa madini, uchakataji wa kimitambo, na usanifu wa kimetalojia.

Imejijengea sifa kwa kuunganisha usahihi wa kisayansi na uelewa wa ndani wa mazingira, ikiwasaidia wachimbaji wadogo hadi makampuni makubwa kuongeza thamani ya rasilimali zao. Kupitia ubunifu, mafunzo, na utaalamu wa kina, imeendelea kujitoa kuinua sekta ya madini ya Tanzania.

About the author

mzalendoeditor