Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Dkt. Tulia Ackson, leo Juni 26, 2025, ameongoza hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi katika ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wavulana Bunge, inayojengwa katika eneo la Kikombo, jijini Dodoma..
Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika saa 7 mchana, Dkt. Tulia amesema mradi huo ni ushahidi wa dhamira ya pamoja ya wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuwekeza kwenye elimu bora na ya maadili kwa vizazi vijavyo, bila kujali jiografia ya majimbo yao.
“Fedha za awali zilizowezesha kuanza kwa ujenzi huu ni mchango wa waheshimiwa wabunge kupitia posho zao,Wamechangia kwa moyo mmoja, bila kuangalia kwamba shule inajengwa Dodoma,” amesema Spika Tulia kwa kupongeza mshikamano huo wa bunge.
Ameeleza kuwa hatua hiyo inatokana na maono ya muda mrefu ya kuwa na shule ya pekee itakayolea viongozi wa kesho kwa misingi ya maadili, nidhamu, na uzalendo, ikiwemo kukuza elimu ya kisayansi na uongozi bora miongoni mwa Wavulana.
Spika ameongeza kuwa sehemu nyingine ya fedha na vifaa ni mchango wa wadau mbalimbali waliokuwa wakishiriki katika matukio kama Bunge Bonanza pamoja na marafiki wa maendeleo walioguswa na dhamira hiyo ya kitaifa.
“Tunawashukuru sana wabunge na wadau wote waliotuunga mkono katika hatua ya awali,tunawaomba waendelee kushirikiana nasi kwa kuchangia fedha, vifaa vya ujenzi, au hata ushauri wa kitaalamu,” amesema.
Ujenzi wa shule hiyo unatarajiwa kuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo ya elimu jijini Dodoma, sambamba na kuongeza nafasi za wavulana kupata mazingira bora ya kujifunza, kuishi, na kukuza vipaji vyao kitaaluma na kijamii.
Ameeleza kuwa Taasisi hiyo ya elimu italeta manufaa ya muda mrefu kwa taifa, kwani itakuwa chimbuko la viongozi, wataalamu, na wajasiriamali watakaolijenga taifa katika karne ya sasa na zinazokuja.
Dkt.Tulia amewahimiza wananchi, Taasisi binafsi, mashirika ya umma na wadau wa maendeleo kujitokeza kwa wingi kuunga mkono ujenzi wa shule hiyo kama sehemu ya jukumu la pamoja la kuimarisha elimu nchini.
“Maendeleo hayawezi kusukumwa na Serikali peke yake,tunahitaji moyo wa kujitolea, mshikamano, na uzalendo wa vitendo kutoka kwa kila mmoja wetu,” amesisitiza Dtk.Tulia