Featured Kitaifa

AMREF TANZANIA YAUNGANA NA WADAU KATIKA MAPAMBANO DHIDI YA DAWA ZA KULEVYA – DODOMA

Written by mzalendoeditor



Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Bw. Aretas Lyimo (kushoto), akikabidhi cheti cha ushiriki kwa mwakilishi wa Amref Tanzania, Bi. Emma John, Mshauri wa Jamii wa Masuala ya VVU, ikiwa ni ishara ya kutambua mchango wa taasisi hiyo katika mapambano dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya nchini. Tukio hilo lilifanyika katika kilele cha Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya kwa mwaka 2025, yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre, jijini Dodoma.



Dkt. George Mgomela, Mkurugenzi wa Miradi, U.S CDC Tanzania, akipata maelezo kutoka kwa watendaji wa Amref Tanzania alipotembelea banda lao katika Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre, jijini Dodoma.

 

Katika ziara hiyo, Dkt. Mgomela ameelezwa kuhusu huduma ya MAT na mbinu za kupunguza madhara kwa watumiaji wa dawa za kulevya, zinazotekelezwa na Amref Tanzania kupitia ufadhili Serikali ya Marekani(PEPFAR) kupitia CDC Tanzania, ikiwa ni sehemu ya mapambano dhidi ya VVU Visiwani Zanzibar.

Wafanyakazi wa Amref Tanzania pamoja na wadau mbalimbali wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya kwa mwaka 2025, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre, jijini Dodoma.

Wafanyakazi wa Amref Health Africa Tanzania wakiwa katika picha ya pamoja wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya kwa mwaka 2025, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre, jijini Dodoma.

 

Dodoma, Juni 26, 2025 – Amref Health Africa – Tanzania, kupitia ufadhili wa Serikali ya Marekani chini ya Mpango wa PEPFAR kupitia Kituo cha Serikali ya Marekani cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC Tanzania), imeungana na Serikali ya Tanzania na wadau mbalimbali katika kuadhimisha kilele cha Siku ya Kupiga Vita Matumizi ya Dawa za Kulevya, kilichofanyika kitaifa jijini Dodoma.

 

Maadhimisho hayo yamefanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Convention Centre, yakiongozwa na kauli mbiu: “Wekeza kwenye kinga na Tiba Dhidi ya dawa za Kulevya.” Tukio hilo liliwakutanisha viongozi wa kitaifa, mashirika ya kiraia, wataalam wa afya, na wanufaika wa miradi ili kuongeza uelewa na kuhamasisha mshikamano katika mapambano dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya.

 

Amref Tanzania imekuwa mshirika wa muda mrefu katika jitihada za kupambana na matumizi ya dawa za kulevya na athari zake, hususan kwa kushirikiana na Wizara ya Afya Zanzibar, Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (ZDCEA) na wadau wengine. Kupitia mradi huu, Amref inatekeleza afua za kiafya zenye lengo la kusaidia waraibu wa dawa za kulevya, kupunguza madhara, na pia kupunguza maambukizi ya VVU/UKIMWI ambayo mara nyingi huambatana na matumizi ya sindano zisizo salama.

 

Kwa kushirikiana na wadau hawa, Amref Tanzania inatoa huduma za Medication Assisted Treatment (MAT) kupitia Kituo cha Kidongo Chekundu, Zanzibar, ambapo waraibu hupata tiba mbadala salama, ushauri nasaha, pamoja na ufuatiliaji wa kiafya. Huduma hizi zimekuwa mkombozi kwa mamia ya wanufaika waliokuwa katika mzunguko wa uraibu na sasa wameweza kurejea katika maisha ya heshima na tija.

 

Katika maadhimisho hayo ya kitaifa, Amref Tanzania imepata fursa ya kushiriki kwa kuweka banda la maonesho, ambapo wananchi walipata elimu kuhusu madhara ya dawa za kulevya, huduma za MAT, pamoja na mafanikio ya wanufaika wa huduma hizo. Baadhi ya wanufaika wa mradi waliweza kushiriki moja kwa moja na kutoa ushuhuda wa maisha yao kabla na baada ya huduma hizo, wakisisitiza kuwa uraibu unaweza kutibika ikiwa msaada sahihi utatolewa kwa wakati.

 

Nilikuwa nimepoteza kabisa mwelekeo wa maisha yangu. Matumizi ya dawa yalikuwa yamenifanya nihisi kama maisha yangu hayana tena maana. Lakini baada ya kuanza tiba ya MAT na msaada kutoka kwa wadau, sasa ninafanya kazi, nimekuwa baba bora kwa watoto wangu, na nimeanza maisha mapya,” alisema Amki (Siyo jina lake halisi), mnufaika wa programu.

 

Mgeni Rasmi, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya, aliwataka wadau wote kuongeza mshikamano, kushirikiana kwa karibu, na kuwekeza katika mikakati endelevu itakayosaidia kutokomeza kabisa matumizi ya dawa za kulevya nchini Zanzibar na Tanzania Bara kwa ujumla.

 

Aidha, Waziri Mkuu alisisitiza kuwa ni muhimu kuendeleza juhudi za pamoja, za kina na endelevu ili kuhakikisha mafanikio ya kudumu katika afya na ustawi wa jamii.

 

About the author

mzalendoeditor