Featured Kitaifa

BALOZI NCHIMBI: MAONI YOYOTE KUHUSU AMANI YA TANZANIA HAYATAPUUZWA

Written by mzalendoeditor

*Awahakikishia viongozi wa dini, taasisi za kijamii na kimila

*Awapongeza wanawake kusimamia amani

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi amesema kuwa maoni yoyote yanayolenga kuhakikisha Tanzania inaendelea kudumisha amani na utulivu, hayajawahi kupuuzwa na hayatapuuzwa.

Aidha, Balozi Nchimbi amemwelezea Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa ni kiongozi mwanamke ambaye uongozi wake, umeongeza heshima kubwa kwa wanawake na Tanzania, akiendeleza safari iliyoanzishwa na viongozi wengine wanawake jasiri, tangu wakati wa kudai uhuru na kuiweka Tanzania katika ramani ya dunia.

Balozi Dkt. Nchimbi amesema hayo alipokuwa akifungua Jukwaa la Wanawake wa Arusha 2025, lililowakutanisha wanawake katika kujadili maada ya ‘Safari ya Mwanamke Arusha 2025’, katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC), jijini Arusha, Jumanne, tarehe 24 Juni 2025.

“Hivyo ndivyo wanawake wanalitazama taifa letu (kama wanavyotazama watoto wao). Wanataka nchi yetu iendelee kuwa na amani, nchi yetu iendelee kuwa tulivu. Nataka nitumie nafasi hii, kuwahakikishia wanawake wa Tanzania, kwamba CCM inatambua dhamana yake ya kulinda amani ya nchi yetu. 

“Nataka niwahakikishie viongozi wa mila, viongozi wa dini, viongozi wa taasisi za kijamii, niwahakikishie Watanzania wote, kwamba maoni yenu yanayohusu kuendeleza amani na utulivu katika nchi yetu, hatujawahi kuyapuuza kama Chama Cha Mapinduzi,” alisema Balozi Nchimbi na kuongeza;

“Na tukitambua kuwa amani ndiyo kipaumbele cha kwanza cha mwanamke wa Tanzania…akitambua kwamba kuilinda amani ni kuilinda nchi yetu, kukilinda kizazi cha sasa na kizazi kijacho, tutaendelea kuisimamia amani ya nchi yetu kwa nguvu zetu zote.”

Jukwaa hilo ambalo wazungumzaji wakuu wa mada hiyo walikuwa ni pamoja na Mama Fatma Karume, mjane wa Hayati Mzee Abeid Amani Karume, Mama Anne Makinda, Dkt. Asha-rose Migiro, Bi. Zakhia Meghji, na wanawake wengine vijana, lililenga kuzungumzia safari ya mwanamke katika nyanja mbalimbali za maisha, kisiasa, kiuchumi na kijamii nchini.  

About the author

mzalendoeditor