Na.Kulwa Meleka-DODOMA
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Carolyne Nombo amezindua rasmi Mfuko wa Ufadhili wa Masomo wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOSO Scholarship Fund) katika hafla iliyofanyika Chuoni hapo, jijini Dodoma.
Akizungumza katika hafla hiyo, Prof. Carolyne Nombo amewapongeza wanafunzi kwa ubunifu wao, amesema amesema uwepo wa Mfuko huo ni ishara ya mafanikio makubwa na mfano bora wa uwajibikaji na ubunifu miongoni mwa vijana wa Kitanzania katika kusaidiana
Mfuko huu, ambao ni matokeo ya jitihada za Serikali ya Wanafunzi ya mwaka wa 2024/2025, unalenga kuwasaidia wanafunzi wenye changamoto za kifedha kuendelea na masomo yao. Mfuko huo utaendeshwa kupitia uwekezaji wa shilingi milioni 100 katika hati fungani ya Benki Kuu ya Tanzania (BOT), hatua inayosifiwa kama mfano wa nidhamu ya kifedha na maono ya uongozi.
“Hatua hii si msaada wa kawaida bali ni uwekezaji wa muda mrefu kwa kizazi cha viongozi na wataalamu wa kesho.”
Mfuko wa UDOSO Scholarship Fund utawanufaisha wanafunzi 11 kila mwaka kutoka Ndaki, Shule Kuu, na Taasisi mbalimbali za Chuo Kikuu cha Dodoma. Ufadhili huu unalenga kuimarisha juhudi za Serikali za kuwezesha wanafunzi kupata elimu bora, sambamba na jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia Samia Scholarship.
Aidha, Prof. Carolyne Nombo amesifu Serikali ya Wanafunzi kwa kuandaa kanuni za kusimamia mfuko huo, zikilenga uwazi, haki, na uendelevu. Menejimenti ya Chuo Kikuu cha Dodoma pia ilipongezwa kwa kusaidia katika ujenzi wa viongozi wenye maono ya kizalendo na uwajibikaji.
Hata hivyo ametoa wito kwa Taasisi nyingine za elimu nchini kuiga mfano huo
“Ni wajibu wa kila mmoja wetu kushiriki kuhakikisha lengo la mfuko huu linafanikiwa.” amesema
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Prof. Lugano Kusiluka, amepongeza hatua ya Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOSO) kuanzisha hatifungani kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Mpango huo unalenga kuwasaidia wanafunzi wanaokumbwa na changamoto za kifedha, ambazo mara nyingine zinalazimisha baadhi yao kusitisha masomo.
Prof. Kusiluka amesema kuwa mchakato huu ni matokeo ya ushirikiano wa karibu kati ya serikali ya wanafunzi ya awamu iliyopo na iliyopita, bila kuwepo kwa misuguano. Alisema kuwa wazo la kuwasaidia wanafunzi wenzao ni ishara ya upendo wa kweli, unaoendana na utamaduni wa jamii ya Kitanzania.
“Niwaombe wanafunzi wengine wawekeze binafsi hata kama sio wanafunzi, ili kujijengea msingi mzuri wa maisha hata baada ya kuhitimu masomo yao. Kupitia mchakato huu, tunaonesha kuwa vijana wetu wanaelewa umuhimu wa kusaidiana kama taifa. Mfumo huu utasaidia kuokoa maisha ya wanafunzi wengi waliokaribia kusitisha masomo yao kwa sababu ya ukosefu wa fedha,” amesema Prof. Kusiluka.
Amesema kuwa wanafunzi watakaonufaika na mfuko huo watahamasika kusaidia wengine mara wanapopata nafasi ya kujiajiri au kuajiriwa. Aidha, wazo hili limepokelewa kwa furaha kubwa na menejimenti ya chuo hicho, na Baraza la Chuo limebariki mpango huo.
Tunawakaribisha wanafunzi kutoka vyuo vingine waje kujifunza kuhusu wazo hili zuri. Hii ni hatua muhimu kwa maendeleo ya vyuo vyetu na taifa kwa ujumla. Ninaamini litapigiwa chapuo na watanzania wengi,” amesema Prof. Kusiluka.
Awali Rais wa serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOSO) Bi Jackline Humbaro Mfuko wa Ufadhili wa Masomo (UDOSO Scholarship Fund) umeanzishwa kwa lengo la kusaidia wanafunzi wenye uhitaji, kugharamia miradi ya maendeleo, na kuhakikisha rasilimali za kifedha zinapatikana kwa njia endelevu. Mfuko huo umeanzishwa kwa uwekezaji wa Tsh. milioni 100 kwenye Hati Fungani za Benki Kuu ya Tanzania (BOT), hatua inayotarajiwa kutoa faida ya Tsh. milioni 15.49 kila mwaka hadi 2039.
Mfuko huo ulianzishwa baada ya kupitishwa na Baraza la Mawaziri la UDOSO, Bunge la Jumuiya ya Wanafunzi, Kamati ya Huduma za Ustawi, na Baraza la Chuo Kikuu cha Dodoma. Uwekezaji unafanywa kupitia Benki ya CRDB kama wakala wa BOT, ukilenga kuboresha ustawi wa wanafunzi na kufanikisha miradi ya kijamii chuoni, amesema