Featured Kitaifa

OFISI YA WAZIRI MKUU-SERA,BUNGE NA URATIBU YATOA ELIMU KWA WANANCHI KATIKA WIKI YA UTUMISHI WA UMMA

Written by mzalendoeditor
Mkurugenzi wa Idara ya Uwezeshaji Kiuchumi na Maendeleo ya Sekta Binafsi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge na Uratibu Bw.Conrad  Millinga, akizungumza na Waandishi wa habari katika Banda la Ofisi hiyo wakati wa Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyomalizika Leo Juni 23,2025 katika Viwanja vya Chinangali Park Jijini Dodoma.
Na Alex Sonna, Dodoma
OFISI  ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge na Uratibu imesema imeendelea kuelimisha jamii kuhusu matumizi sahihi ya alama za Taifa zikiwemo Bendera ya Taifa, Wimbo wa Taifa na Ngao ya Taifa, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma iliyofanyika kuanzia Juni 16 hadi Juni 23, 2025.
Akizungumza jijini Dodoma,Mkurugenzi wa Idara ya Uwezeshaji Kiuchumi na Maendeleo ya Sekta Binafsi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge na Uratibu Bw.Conrad  Millinga, amesema baadhi ya taasisi na watu binafsi wamekuwa wakitumia alama hizo kinyume na taratibu zilizowekwa na serikali.
“Tumeona matumizi yasiyo sahihi ya alama hizi muhimu,kwa mfano, wimbo wa taifa mara nyingi hauimbwi kwa ukamilifu wake,tunasisitiza kuwa unatakiwa kuimbwa kwa beti zote mbili kama ilivyoainishwa, na pia matumizi ya rangi na michoro ya bendera au ngao lazima yaendane na muundo rasmi,” amesema Millinga.
Aidha, Mkurugenzi huyo amebainisha kuwa katika kipindi hicho cha wiki ya utumishi wa umma wananchi walipata elimu kuhusu mifuko ya uwezeshaji kiuchumi, programu za kitaifa za maendeleo, na sera mbalimbali za uchumi ambazo zinalenga kuwawezesha Watanzania kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji na kuinua kipato chao.
“Tumetoa elimu kuhusu fursa zilizopo kupitia mifuko hii na namna Watanzania wanavyoweza kunufaika. Lengo ni kuwajengea uelewa wa kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa,” ameongeza.
Pia, Millinga ameeleza kuwa wananchi walielimishwa kuhusu Idara ya Menejimenti ya Maafa ambayo sasa inatekeleza sera mpya ya mwaka 2025 inayotoa mwongozo wa namna sekta mbalimbali zinavyopaswa kushirikiana katika kukabiliana na maafa.
 Amesema kuwa idara hiyo ina mfumo wa kisasa wenye uwezo wa kutambua majanga mapema na kutoa tahadhari kwa wananchi kabla ya madhara kutokea.
Vilevile, amesema elimu ilitolewa kuhusu Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini, ambayo kwa sasa inahakikisha shughuli zote za serikali zinafanyiwa ufuatiliaji na tathmini kwa wakati, hatua inayolenga kuongeza uwajibikaji, ufanisi na utoaji wa huduma bora kwa umma.
Katika hatua nyingine, Millinga ametoa wito kwa wananchi kutembelea Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba, yatakayofanyika kuanzia Juni 28 hadi Julai 13, 2025, katika Viwanja vya Sabasaba, Dar es Salaam.
 “Tutakuwa na banda maalum la Ofisi ya Waziri Mkuu, ambalo litaunganisha taasisi zetu zote zikiwemo: Sera, Bunge na Uratibu; Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu. Tutaendelea kutoa elimu kuhusu huduma mbalimbali za serikali,” amesema.

About the author

mzalendoeditor