Featured Kitaifa

MAJALIWA ATOA SIKU 38 TAASISI ZA UMMA KUJIUNGA MFUMO GovESB

Written by mzalendoeditor

 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza alipomwakilisha  Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kilele cha Wiki ya Utumishi wa Umma  kwenye Viwanja vya Chanangali jijini Dodoma, Juni 23, 2025.  (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ameziagiza taasisi za Serikali ambazo hazijajiunga na mfumo wa kielektroni utakaowezesha mifumo ya Serikali kuwasiliana (GovESB) kujiunga na mfumo huo ifikapo Julai 30 mwaka huu ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia katika kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.

Ametoa maagizo hayo leo Jumatatu (Juni 23, 2025) alipomwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Utumishi wa Umma yaliyofanyika katika viwanja vya Chinangali Park Jijini Dodoma.

“Taasisi zote za umma ambazo hazijajiunga na mfumo huu mwisho ni Julai 30 mwaka huu, wote muwe mmeshaingia pale GovESB, huu ni msisitizo ambao ulitolewa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia pindi eGA watakapokamilisha kila taasisi ipeleke mfumo wake, idadi ya taasisi zilizounganishwa ni chache, hakuna gharama na hutakiwi kupanga bajeti”

Ameongeza kuwa mfumo huo unafaida kubwa katika utumishi wa umma kwani utasaidia kurahisisha utendaji, kutoa taarifa kwa wakati, kuondoa makosa ya kibinadamu katika kuwahudumia wananchi pamoja na kuwabana wala rushwa. “Nimefurahi kujulishwa kwamba jumla ya mifumo 223 kutoka kwenye taasisi 185 imeunganishwa na kusomana”.

Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa taasisi zote za umma zenye mifumo na zinazoendelea kubuni mifumo zihakikishe mifumo hiyo inasomana na inaweza kubadilishana taarifa kupitia mfumo huo wa GovESB ikiwa ni njia mojawapo ya kuendelea kuboresha huduma za Serikali.

Kadhalika Mheshimiwa Majaliwa ameitaka Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) kuhakikisha mifumo iliyounganishwa inaendelea kubadilishana taarifa. “Lakini pia kila anayeingia jiridhishe kuwa anaweza kuwasiliana na wengine wote waliomo ndani, mmenieleza na mmesema kwamba ndivyo ilivyo, nasisitiza kwamba hakikisheni hiyo mifumo inasomana na inabadilishana taarifa”

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Waziri Mkuu ametoa wito kwa watumishi wa umma kuzingatia miiko na maadili ya utumishi katika utekelezaji wa majukumu yao kwa kuzingitia Sera na Sheria kwa manufaa na maendeleo ya Taifa letu. “Nitumie nafasi hii kuwapongeza sana watumishi wote wa umma nchini, niwahikishie kuwa serikali ya awamu ya sita iko pamoja nanyi. “Fanyeni hivyo kwa ajili ya manufaa na maendeleo ya Taifa letu”.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi-Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora George Simbachawene amesema Tanzania imetambulika kimataifa ambapo mwaka 2022 Benki ya Dunia ilifanya utafiti kuhusu ukomavu wa matumizi ya teknolojia duniani katika utoaji wa huduma za Serikali na ushirikishwaji wa wananchi.

Amefafanua kuwa ripoti ya utafiti huo iliyotolewa Machi, 2023 ilibanisha kuwa Tanzania imefanikiwa kupanda daraja kutoka kundi B hadi kundi A na kushika nafasi ya 26 duniani, nafasi ya 2 Afrika na nafasi ya kwanza katika nchi za Afrika Mashariki.

Katika tukio hilo, Mheshimiwa Majaliwa alizindua mifumo miwili ambayo ni Mfumo wa kielektroni unaowezesha mifumo ya Serikali kuwasiliana na kubadilishana taarifa ujulikanao kama Government Enterprises Service Bus (GovESB) Pamoja na Mfumo wa e-Wekeza unaomuwezesha Mtumishi wa Umma kuwekeza katika Mfuko wa Faida (Faida Fund).

Siku ya Utumishi wa Umma husherehekewa Juni 23 kila mwaka na nchi wanachama wa Umoja wa Afrika kwa lengo la kutambua mchango wa Watumishi wa Umma katika maendeleo ya nchi zao na Bara la Afrika kwa ujumla.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Mwandishi wa Taarifa Rasmi za Bunge, Patson Sobha alipotembelea banda la maonesho la Bunge  alipomwakilisha  Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Kilele cha Wiki ya Utumishi wa Umma  kwenye Viwanja vya Chanangali jijini Dodoma, Juni 23, 2025.  Kushoto ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachaweni. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Kaimu Mkurungenzi Mtendaji wa Watumishi Housing, Stephanie Solomon (wa tatu kushoto) alipotembelea banda la maonesho la Watumishi Housing wakati alipomwakilisha  Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Kilele cha Wiki ya Utumishi wa Umma  kwenye Viwanja vya Chanangali jijini Dodoma, Juni 23, 2025.  Wa pili kulia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimsikiliza, Afisa Tehama wa  Mamlaka ya  Serikali Mtandao, Khadija Mzenzi wakati alipotembelea banda la maonesho la mamlaka hiyo alipomwakilisha  Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kilele cha Wiki ya Utumishi wa Umma  kwenye Viwanja vya Chinangali jijini Dodoma, Juni 23, 2025. Kulia kwake ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene na kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama nyaraka za Maendeleo ya Watumishi  kwa Mwaka zilizoandikwa kwa lugha ya kiswahili  alipotembelea mabanda ya maonesho  wakati alipomwakilisha  Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kilele cha Wiki ya Utumishi wa Umma  kwenye Viwanja vya Chanangali jijini Dodoma, Juni 23, 2025. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza alipomwakilisha  Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kilele cha Wiki ya Utumishi wa Umma  kwenye Viwanja vya Chanangali jijini Dodoma, Juni 23, 2025.  (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

About the author

mzalendoeditor