Featured Kitaifa

WADAU WAALIKWA KUTOA MAONI YA KODI KUPITIA MFUMO WA KIELEKTRONIKI

Written by mzalendoeditor


Afisa Usimamizi wa Fedha Mwandamizi, Idara wa Uchambuzi wa Sera, Wizara ya Fedha, Bw. Daved Massawe akitoa elimu kwa Bi. Zainabu Kyama kuhusu huduma zinazotolewa katika Banda la Wizara ya Fedha, kwenye Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, viwanja vya Chinangali, jijini Dodoma.

Afisa Kumbukumbu, Kitengo cha Pension, Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali, Bi. Stella Mtally akitoa elimu kuhusu Pensheni inayolipwa na Hazina kwa Wastaafu kwa Mkazi wa Dodoma Bw. Andrew Madeha, alipotembelea Banda la Wizara ya Fedha, katika Wiki ya Utumishi wa Umma, viwanja vya Chinangali, jijini Dodoma.

Afisa TEHAMA, Idara ya Mifumo ya Kifedha, Wizara ya Fedha, Bi. Zaina Mwanga akitoa elimu kwa Bi. Sophia Matara kuhusu maelekezo ya matumizi ya Aplikesheni ya Mfumo wa Malipo ya Serikali kwa njia ya Kielektroniki wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, viwanja vya Chinangali, jijini Dodoma.

Afisa Usimamizi wa Fedha, Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Bi. Grace Samwel, akitoa elimu ya fedha kuhusu uwekaji akiba, uwekezaji na matumizi kwa wakazi wa Dodoma waliotembelea Banda la Wizara ya Fedha, Wiki ya Utumishi wa Umma, viwanja vya Chinangali, jijini Dodoma.

Afisa Msimamizi wa Fedha, Idara ya Usimamizi wa Bajeti ya Serikali, Wizara ya Fedha, Bw. James Kamomonge, akitoa elimu kuhusu maandalizi ya bajeti ya Serikali na Usimamizi wake kwa Bw. Emmanuel John, alipotembelea Banda la Wizara ya Fedha, kwenye Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayofanyika katika Viwanja vya Chinangali, jijini Dodoma.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Fedha,Dodoma)

Na. Josephine Majura na Chedaiwe Msuya, WF, Dodoma

Wizara ya Fedha imetoa wito kwa wananchi kujenga mazoea ya kushiriki mchakato wa kutoa maoni ya maboresho ya mfumo wa kodi kupitia mfumo wa kieletroniki wa kuwasilisha maoni (Maoni Portal) ili Serikali iweze kuyafanyia kazi kwa maendeleo ya uchumi wa nchi.

Wito huo umetolewa na Afisa Usimamizi wa Fedha Mwandamizi, Idara ya Uchambuzi wa Sera, Wizara ya Fedha, Bw. David Massawe, wakati akitoa elimu ya masuala ya kodi kwa watu waliotembelea Banda la Wizara ya Fedha, wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma katika Viwanja vya Chinangali, jijini Dodoma.

“Mwezi Desemba kila mwaka, Serikali kupitia Wizara ya Fedha hutoa fursa kwa wananchi kupitia dirisha la mfumo wa kieletroniki wa maoni portal ambapo wananchi hualikwa kuwasilisha maoni ya kuboresha mfumo wa kodi ili kuhakikisha kuwa sera za kodi nchini zinazingatia kanuni za usawa, ufanisi, kuakisi matakwa ya wananchi na zenye kuendana na mazingira halisi ya kiuchumi nchini” alisema Bw. Massawe.

Aliongeza kuwa makundi mbalimbali yakiwemo taasisi binafsi na taasisi za umma, wakiwemo wafanyabiashara, wakulima, vijana, wanawake na wastaafu wanashiriki kutoa maoni ili Serikali iweze kuandaa sera za kodi rafiki kwa makundi yote.

Wiki ya Maadhimisho ya Utumishi wa Umma imeanza Juni 16 na inatarajiwa kuhitimishwa Juni 23 mwaka huu ikiwa na kauli mbiu ya “Himiza Matumizi ya Mifumo ya Kidigiti ili kuongeza Upatikanaji wa Taarifa na Kuchangia Uwajibikaji”.

About the author

mzalendoeditor