Vikundi 12 kati ya 126 vilivyokabidhiwa kwa Benki ya CRDB na Halmashauri ya Jiji la Dodoma kwa ajili ya kupitia mchakato wa kupewa mikopo ya asilimia 10 kutoka Serikali, ndivyo vilivyokidhi vigezo na kuendelea na hatua za kupatiwa mikopo hiyo.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Joseph Fungo, katika semina ya mafunzo iliyoandaliwa na Benki ya CRDB kwa ajili ya vikundi vilivyokidhi masharti hayo, baada ya Serikali kusitisha utoaji wa mikopo kupitia halmashauri na kuzielekeza benki zilizoidhinishwa kusimamia mchakato huo.
Kwa mujibu wa Fungo, bado vikundi 467 vinatafutwa na halmashauri kwa kushindwa kurejesha mikopo waliyopewa awali kupitia mpango huo wa asilimia 10 kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, huku kiasi cha shilingi bilioni 1.2 kikiwa hakijarejeshwa.
“Fedha hizi ni deni. Zilikuwa kwa ajili ya kusaidia makundi maalum kujiendeleza kiuchumi. Lakini baadhi ya vikundi vimekimbia na fedha hizo, hivyo tunavifuatilia ili virejeshe mikopo hiyo,” amesema Fungo.
Ameongeza kuwa, kwa sasa halmashauri hiyo imetenga shilingi bilioni 7 kwa ajili ya mikopo hiyo, itakayotolewa kwa vikundi vitakavyopitia mchakato wa uhakiki na kuthibitishwa na CRDB Benki.
Aidha, vikundi vilivyokosa sifa vimekutwa na changamoto mbalimbali zikiwemo utofauti wa taarifa, biashara zisizokidhi masharti ya mkopo waliotaka, pamoja na uelewa mdogo wa usimamizi wa fedha.
“Naomba mliokidhi vigezo muwe waaminifu na muirejeshe mikopo kwa wakati. Hii itasaidia mfumo kuwa endelevu na kuwafikia wengine,” ameongeza Fungo.
Naye Mkuu wa Idara ya Biashara kutoka CRDB Benki Foundation, Fadhili Bushagoma, amesema benki hiyo kwa kushirikiana na halmashauri imetembelea vikundi vyote 126, lakini hadi sasa ni 12 tu ndivyo vimekidhi vigezo.
“Wengine bado wana nafasi ya kurekebisha kasoro walizobainika nazo ili wapate fursa hiyo,” amesema Bushagoma.
Kwa upande wake, Bahati Atanasio kutoka Kikundi cha Vijana wa Kata ya Chihanga, ameishauri Serikali kuhakikisha inatoa mikopo kulingana na kiwango kilichoombwa, ili kusaidia utekelezaji wa malengo ya vikundi.
“Wengi hukimbia na mikopo kwa sababu wanapewa kiasi kidogo tofauti na walichoomba. Hii huleta migogoro ndani ya vikundi na wengine hutoroka bila kurejesha,” amesema Atanasio.
Serikali ilisitisha utoaji wa mikopo hiyo kupitia halmashauri na kuelekeza benki zilizoidhinishwa, ili kuhakikisha kuwa walengwa wanaopokea mikopo ni wale wanaokidhi vigezo kwa mujibu wa wataalamu wa fedha.