Featured Kitaifa

NAIBU WAZIRI UTALII NA UTUMISHI WAIPONGEZA REA KAMPENI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA

Written by mzalendoeditor

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula na Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu wameupongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kutekeleza kampeni ya Nishati Safi ya Kupikia kwa vitendo.

Viongozi hao wametoa pongezi hizo leo Juni 20, 2025 kwa nyakati tofauti walipotembelea banda la Wakala huo katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika viwanja vya Chinangali, Jijini Dodoma.

“Kwanza niwapongeze REA kwa kushiriki katika Maadhimisho haya ambapo wananchi wanaweza kupata taarifa juu ya miradi mbalimbali mnayoitekeleza ambayo imelenga kuboresha maisha ya yao.

Pia niwapongeze kwa kazi kubwa mnayofanya ya kufikishia wananchi umeme vijijini. Kwa kweli mnafanya kazi kubwa sana. Na hili la nishati safi ya kupikia ambayo ni ajenda ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan mmelitendea haki. Muendelee kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa nishati safi ya kupikia ili tuondokane na uharibifu wa kimazingira unaofanyika kwa watu kukata miti kwa ajili ya kupikia,” amesema Mhe. Sangu.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Kitandula amesema kuwa matumizi ya nishati safi ya kupikia licha ya kuokoa afya za Watanzania, pia itawezesha kutunza mazingira.

“Wizara ya Maliasili na Utalii limepewa jukumu la kulinda rasilimali misitu. Na kama mnavyofahamu kumekuwa na changamoto kubwa sana ya ukataji miti hovyo hali iliyopelekea kupata changamoto ya mabadiliko ya tabianchi. Tunamshkuru sana Mhe. Rais ameliona hilo na kuamua kuja na Mkakati wa matumizi ya nishati safi na salama.

Matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia haitasaidia tuu kuokoa maisha ya kina mama waliokuwa wanapoteza maisha kwa kutumia nishati isiyo safi na salama ya kupikia. Pia itaokoa mazingira yetu. Tuwapongeze REA kwa miradi mbalimbali inayotekeleza ya kuhamasisha matumizi ya nishati ya kupikia. Niendelee kutoa rai kwa Watanzania kuitikia kampeni hii ya kutumia nishati safi na salama ya kupikia ili Taifa letu liendelee kubaki salama,” amesema Mhe. Kitandula.

Wakala wa Nishati Vijijini (REA) unashiriki katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kwa kutoa elimu mbalimbali ikiwamo elimu juu ya nishati safi ya kupikia ikiwa ni utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia ambao una lengo la kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia kufikia asilimia 80 ifikapo 2034.

About the author

mzalendoeditor