Na.Alex Sonna– Dodoma
Serikali imezidi kufungua milango ya maarifa kwa wananchi kuhusu mustakabali wa taifa, kupitia utoaji wa elimu wa moja kwa moja unaofanyika kwenye Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma. Kupitia Kliniki za Papo kwa Hapo, wananchi wamepewa nafasi ya kuelewa mipango mikubwa ya taifa, ikiwemo Dira ya Maendeleo ya 2050.
Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Dkt. Tausi Kida, amesema kuwa zaidi ya wananchi 100 tayari wametembelea banda la ofisi hiyo, wakionyesha kiu ya kujua kwa undani majukumu ya taasisi hiyo mpya na mwelekeo wa maendeleo ya nchi.
“Tumeimarisha Kliniki zetu za papo kwa hapo ili kutoa elimu moja kwa moja. Wananchi wanaonyesha hamasa kubwa ya kujua dira ya 2050 na nafasi ya sekta binafsi katika kufanikisha uchumi wa mafanikio,” amesema Dkt. Kida.
Dkt. Kida ameeleza kuwa rasimu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050 ipo katika hatua ya mwisho ya maandalizi, na itawasilishwa Bungeni tarehe 26 Juni 2025, ambako itapitiwa na kuridhiwa kabla ya kuzinduliwa rasmi na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan.
“Hii dira itakuwa msingi wa mipango ya muda mrefu, na tutaiambatanisha na mpango wa utekelezaji utakaofafanua jinsi tutakavyofikia maono hayo ya Taifa,” amesema
Kwa upande wake Mchumi wa Ofisi hiyo Octavian Ruta katika kusisitiza umuhimu wa ushiriki wa sekta binafsi,amesema Serikali inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na ina sera mpya ya uwekezaji inayotambua mwekezaji si kwa uraia, bali kwa mtaji, ajira anazotoa na mchango wake katika pato la Taifa.
“Lazima sekta binafsi iwe injini ya kukuza uchumi. Wawekezaji wa ndani wapewe nafasi ya kuwekeza kwa wingi, kwa sababu maendeleo ya kweli yanahitaji nguvu ya pamoja,” amesema.
Akizungumzia dhamira ya ofisi yake,Ruta amesema kuwa jukumu kubwa ni kuratibu mipango mikubwa ya maendeleo, kuhakikisha kwamba kila hatua ya kupanga inazingatia maslahi mapana ya taifa na vizazi vijavyo.
“Tunahitaji kuwa na Taifa linaloongozwa kwa mwelekeo thabiti. Dira ya 2050 si tu karatasi, bali ni matumaini ya Watanzania kwa uchumi shindani, jumuishi na wenye ustahimilivu,” amehitimisha.