Featured Michezo

WANAFUNZI UDOM WANG’ARA MASHINDANO YA TEKNOLOJIA YA HUAWEI NCHINI CHINA

Written by mzalendoeditor

 

Na.Kulwa Meleka – Dodoma

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Prof. Lugano Kusiluka, amewapongeza wanafunzi wanne kutoka Ndaki ya Sayansi ya Kompyuta na Elimu Angavu kwa ushindi walioupata katika mashindano ya teknolojia yaliyoandaliwa na kampuni ya Huawei, yaliyofanyika Shenzhen, China.

Hafla ya kuwapongeza wanafunzi hao ilifanyika tarehe 18 Juni 2025, katika ofisi za Utawala Mkuu wa chuo hicho.

“Niliwakabidhi bendera ya Tanzania na ya Chuo Kikuu cha Dodoma nikiwaagiza mrudi na ushindi, na mmefanya hivyo. Ushindi huu ni wa kihistoria kwa UDOM na kwa nchi yetu. Mmeonyesha ulimwengu kuwa Tanzania inaweza kushindana na kushinda katika masuala ya teknolojia licha ya changamoto za ukuaji,” alisema Prof. Kusiluka.

Amesema ushindi huo umefungua milango kwa wanafunzi wengine kushiriki mashindano ya kimataifa, huku akiipongeza Ndaki ya Sayansi ya Kompyuta na Elimu Angavu kwa kuendelea kushiriki kikamilifu katika mashindano ya TEHAMA, ambapo UDOM imekuwa ikipata mafanikio ya juu mara kwa mara.

“Tunaendelea kuimarisha elimu na mafunzo ili kuandaa wanafunzi wenye ujuzi na maarifa ya kisasa. Mafanikio haya yanadhihirisha ubora wa mitaala yetu na juhudi za walimu wetu. Tutaheshimiwa si kwa vyeti pekee, bali kwa maarifa na ujuzi tulioupata,” aliongeza Prof. Kusiluka.

Ameeleza kuwa chuo hicho kinatarajia kuanzisha kituo cha utafiti wa teknolojia za kidijitali kwa kushirikiana na Tume ya TEHAMA ya Taifa ndani ya miezi sita ijayo. Pia, chuo kimepokea msaada wa kuboresha maabara ya usalama wa kimtandao kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

“Tumekubaliana pia na Benki ya NMB kufanya kazi ya utafiti na kutoa mafunzo katika teknolojia za kidijitali. Wadau wanazidi kuongezeka, na hii inafungua fursa si kwa UDOM pekee, bali kwa Watanzania wote,” alisema Prof. Kusiluka.

Aidha, aliwapongeza wanafunzi kutoka vyuo vingine vya Tanzania walioshiriki mashindano hayo kwa kushirikiana na wenzao kutoka UDOM, na kuhimiza kuendeleza ushirikiano huo katika maeneo mengine ya kitaaluma na kimaendeleo.

Kwa upande wake, Kaimu Rasi wa Ndaki ya Sayansi ya Kompyuta na Elimu Angavu, Dkt. Florence Rashidi, alisema zaidi ya wanafunzi 300 walishiriki mchujo wa awali uliofanyika UDOM, na hatimaye wanne walichaguliwa kushiriki ngazi ya kimataifa. Mmoja kati yao aliibuka mshindi wa kwanza katika kipengele cha Network Track.

Paul Nkingwa, mmoja wa washindi, alisema kuwa mashindano yalikuwa ya vitendo na yalifanyika bila mtandao, huku mitihani ya awali ikichukua saa nne na ile ya ngazi ya kimataifa ikichukua saa nane.

Katika hotuba yake ya kufunga hafla hiyo, Prof. Kusiluka aliwahimiza wanafunzi wa UDOM na vijana kote nchini kutumia fursa zinazotolewa na mashindano ya kimataifa ili kuongeza maarifa na ujuzi.

“Tunaungana na juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuimarisha mifumo ya TEHAMA na matumizi ya teknolojia kwa maendeleo ya taifa,” alihitimisha Prof. Kusiluka.





About the author

mzalendoeditor