Featured Kitaifa

WAZIRI SIMBACHAWENE ATEMBELEA BANDA LA MIPANGO NA UWEKEZAJI

Written by mzalendo

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene ametembelea na kukagua banda la tume ya taifa ya Mipango na Uwekezaji katika maonesho ya wiki ya utumishi wa umma yanayofanyika katika viwanja vya Chinangari Park Dodoma.

Akitoa maelezo mbele ya Waziri huyo leo Juni 17,2025 Mkuu wa Kitengo cha Habari na mawasiliano Serikalini Raymond Mtani amesema ofisi hiyo ina jukumu la kuratibu mipango ya kitaifa na kusimamia shughuli za sekta za uwekezaji wa ndani.

“Tangu kuanzishwa kwake ofisi hii imekuwa na mafanikio makubwa, katika mpango wa kitaifa imeratibu zoezi kubwa la uandikaji wa dira ya taifa ya 2050 ambapo mchakato huo ulishirikisha wananchi wote zaidi ya Milioni 1 ambao walitoa maoni yao na waliyaridhia,”amesema.

Aidha, ameongeza kuwa kwasasa wanalo zoezi la kuandaa mpango wa pili wa maboresho ya mazingira ya biashara.

“Hili ni zoezi muhimu kwasababu tunakwenda kwenye uchumi wa Trilioni moja kwa maono ya dira ya taifa ya 2050, kwahiyo sekta binafsi zinatarajiwa kuchangia zaidi ya asilimia 50 ili tuweze kufikia hayo malengo,”ameongeza.

Wiki ya Utumishi kitaifa imeanza Juni 6 mpaka Juni 23,2025 ikiwa inajumuisha taasisi na Wizara mbalimbali hapa nchini.

About the author

mzalendo