Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati wa Maadhimisho ya Miaka 21 ya Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu (TAHLISO) yaliyofanyika leo Juni 14,2025 kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma
Na.Alex Sonna-DODOMA
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa,amewataka wanafunzi wa Vyuo Vikuu na Vya Kati kuhakikisha Taifa linaendelea kuwa Tulivu lenye amani na Mshikamano kama ilivyoasisiwa na Hayati Baba wa Taifa Julius Kambarage Nyerere na Abeid Aman Karume katika kuelekea uchaguzi Mkuu wa Mwaka huu.
Waziri Mkuu ameyasema hayo lei Juni 14,2025 wakati wa maadhimisho ya miaka 21 ya Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu, yaliyofanyika katika uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma
“Natoa wito kwa wanavyuo wote nchini kutokubali kutumika na baadhi ya wanasiasa wenye nia ovu ya kuwavuruga na kilifanya Taifa liishi bila amani “Tanzania ni yetu, endeleeni kuhakikisha kuwa Taifa hili linabaki salama pamoja na uchaguzi tulionao mbele yetu”amesema
Aidha Mhe.Majaliwa amewatahadharisha dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya na vitendo vinavyokwenda kinyume na maadili.
“Katika siku za hivi karibuni, tumeshuhudia kuongezeka kwa tabia ambayo ni kinyume na maadili na mila yetu ya Kitanzania. Ninakuhimiza kuunga mkono juhudi za serikali katika kuelimisha wanafunzi wenzako dhidi ya mazoea kama vile ushoga, ujamaa, na unyanyasaji wa dawa za kulevya, ambazo zinapingana na maadili yetu ya kitaifa,” amesema Mhe.Majaliwa
Hata hivyo amesema kuwa katika mwaka 2025/2026 Serikali imepanga kutoa mikopo kwa wanafunzi 252,773 wakiwemo 88,320 wa mwaka wa kwanza ili kuwafikia wanafunzi wengi zaidi.
“Huu ni muendelezo wa malengo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuendelea kuboresha elimu ya juu na mazingira ya wanafunzi kwa ujumla, Mwaka 2024/2025, mikopo ya shilingi bilioni 787.4 imetolewa kwa wanafunzi 248,331 ikilinganishwa na bilioni 570 kwa wanafunzi 177,925 mwaka 2021/2022 sawa na ongezeko la asilimia 40”.
Mhe. Majaliwa amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2025/2026 wanafunzi 2,630 watapatiwa Ufadhili wa kupitia progamu hiyo ambayo mpaka sasa jumla ya wanafunzi 1,976 wananufaika na ufadhili huo . “Programu hii ni kwa ajili ya wanafunzi wanaofanya vizuri katika mitihani ya kidato cha Sita katika masomo ya Sayansi”.
Pia amesema ili kuleta unafuu katika urejeshaji wa mikopo, Serikali imeondoa adhabu na tozo ya kulinda thamani katika urejeshaji wa mikopo kwa lengo la kuongeza unafuu kwa wahitimu. “Hatua hii imeongeza marejesho ya mikopo. Vilevile, imetengenezwa Mfumo wa Marejesho unaotumika na taasisi 3,565, na mfumo wa utambuzi unaotumika na wanufaika takriban 3,000 kwa mwezi.”
Aidha amesema kuwa katika mwaka 2023/2024 mpango huo ulianza kwa kutoa mikopo ya shilingi bilioni 7.29 na mwaka 2024/2025 ziliongezwa hadi kufikia shilingi bilioni 19.95 sawa na ongezeko la asilimia 177.6.
“Mpango huu unahusisha fani za kipaumbele ambapo jumla ya wanafunzi 13,214 wamenufaika hadi sasa”
Naye, Naibu Waziri Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Qs Omar Kipanga amesema Wizara hiyo inaendelea na mpango wa kusimamia utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 toleo la 2023 yenye kulenga kutoa elimu inayozingatia ujuzi kulingana na mahitaji ya soko la ajira na kuchangia katika maendeleo ya Taifa.
“Katika kufanikisha utekelezaji wake, tumefanikiwa kuhuisha mitaala na kuandaa miongozi mbalimbali yenye lengo la kuhakikisha elimu inayotolewa nchini inazingatia viwango vya kitaifa, kimataifa na kuwajengea wahitimu ujuzi unaohitajika katika karne ya 21.”
Kwa Upande wake Rais wa Wanafunzi Taasisi za Elimu ya Juu Tanzania (TAHLISO) Geofrey Kiliba amesema kuwa taasisi hiyo inaishukuru Serikali kwa maboresho makubwa katika sekta ya elimu ya juu, Elimu ya Mafunzo na Ufundi Stadi kuanzia miundombinu, kuongezeka kwa bajeti ya mikopo, kuimarisha kwa mitaala na usimamizi bora wa vyuo na taasisi za elimu ya juu
“Sisi TAHLISO tupo tayari kuendelea kushirikiana na Serikali katika nyanja zote ikiwemo kisera na kielimu ili kuchochea maendeleo makubwa zaidi kwa Taifa letu”
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza katika Maadhimisho ya Miaka 21 ya Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu (TAHLISO) kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, Mei 14, 2025. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiteta na Rais wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu (TAHLISO), Geofrey Kiliba katika Maadhiisho ya Miaka 21 ya TAHLISO yaliyofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, Juni 14, 2025. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Baadhi ya washiriki wa Maadhimisho ya Miaka 21 ya Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu (TAHLISO) wakimsikiliza mgeni rasmi Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipozungumza kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, Mei 14, 2025. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waandamanaji wakipita mbele ya mgeni rasmi Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika Maadhimisho ya Miaka 21 ya Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu (TAHLISO) kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, Mei 14, 2025. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na viongozi alipowasili kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma kwa mgeni rasmi Maadhimisho ya Miaka 21 ya Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya Juu (TAHLISO) kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, Mei 14, 2025. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)