Na WMJJWM- Dodoma
Maafisa Habari wa Mikoa wametakiwa kuitangaza kwa nguvu Programu ya Kizazi Chenye Usawa ili kusaidia utekelezaji wa haki na usawa wa kiuchumi nchini.
Wito huo umetolewa jijini Dodoma na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Merkion Ndofi, wakati akizungumza katika kikao cha kuwajengea uelewa Maafisa Habari kuhusu utekelezaji wa programu hiyo.
Ndofi amesema Maafisa Habari ni wadau muhimu katika maeneo yao kwa kuwa ni wasemaji wa miradi mbalimbali ya Serikali na anaamini kupitia wao taarifa kuhusu Programu ya Kizazi Chenye Usawa zitasambaa na kufahamika zaidi kwa jamii.
“Programu hii imekuwepo kwa muda mrefu na sasa inatimiza miaka mitano. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, alishiriki Mkutano wa Kizazi cha Usawa uliofanyika Paris na akaahidi kuwa kinara katika kutekeleza haki na usawa wa kiuchumi,” amesema Ndofi.
Ameongeza kuwa Serikali inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika maeneo manne ya kipaumbele ambayo ni, Uwezeshaji wa kijinsia kwenye sekta binafsi, Kazi zenye staha kwa wanawake katika sekta rasmi na isiyo rasmi,Upatikanaji wa rasilimali za uzalishaji kwa wanawake, na Ubunifu na utekelezaji wa miradi ya kiuchumi kwa wanawake.
“Niwapongeze kwa kujitokeza kushiriki kikao hiki na niwashukuru waajiri wenu kwa kutambua umuhimu wa programu hii. Hii inaonesha wazi kuwa wanathamini nafasi ya habari katika maendeleo,” ameongeza Ndofi
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jinsia katika Badru Abdnoor, amewataka Maafisa Habari kupaza sauti kuhusu Programu ya Kizazi Chenye Usawa ili jamii ifahamu fursa zilizopo na kuweza kushiriki kikamilifu.
Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Juliana Kibonde amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango wa Maafisa Habari, na ndiyo sababu imeamua kuwakutanisha ili kujadiliana kwa pamoja kuhusu namna bora ya kuitangaza programu hiyo kwa ufanisi.
Nao Maafisa Habari hao wamesema baada ya kupata uelewa huo watahakikidja wananchi katika mikoa yao wanaielewa Programu hiyo ili waweze kunufaika na utekelezaji wake hasa katika kuwa na jamii yenye Usawa wa Kijinsia katika nyanja mbalimbali.