Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba bungeni jijini Dodoma leo tarehe 12 Juni 2025 akiwasilisha Hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2025/26 bungeni jijini Dodoma
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis akiwa na Naibu Mawaziri mbalimbali, akishiriki kikao cha Bunge cha uwasilishaji wa Hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2025/26 iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba bungeni jijini Dodoma
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja (wa pili kulia) akiwa na viongozi mbalimbali, akifuatilia kikao cha Bunge cha uwasilishaji wa Hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2025/26 iliyowasilishwa na Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba bungeni jijini Dodoma
…..
Serikali imesema Muungano ni tunu adhimu ambayo imesaidia kuendelea kufikia malengo ya nchi kwa vipindi tofauti tangu kuasisiwa kwake hivyo imewataka Watanzania kuendeleza upendo na mshikamano uliopo.
Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba ameliarifu Bunge wakati akiwasilisha Hotuba ya Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka 2025/26, bungeni jijini Dodoma leo tarehe 12 Juni 2025 ambapo amesema fedha za utekelezaji wa miradi zimepatikana.
Amesema katika kuhakikisha nchi inakuwa na uhimilivu wa kiuchumi dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, inatekeleza programu mbalimbali za uhifadhi wa mazingira.
Mhe. Nchemba amesema kuwa pamoja na masuala mengine programu za uhifadhi wa mazingira zinahusisha maboresho ya sheria, kanuni na taratibu
mbalimbali.
Alifafanua kuwa Serikali imeendelea kunufaika na programu mbalimbali za
uhifadhi wa mazingira kutoka kwa Washirika wa Maendeleo ikiwemo Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kupitia dirisha la Resilience and Sustainability
Facility (RSF).
“Naomba niwahikikishie Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuchukua hatua madhubuti kwa ajili ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi zikiwemo utekelezaji wa Mpango Kabambe wa Taifa wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (2022 – 2032) ambao unalenga kutatua changamoto za mazingira nchini,” alisema.
Dkt. Nchemba aliongeza kuwa Serikali imeanzisha Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC) ili kuimarisha usimamizi na kunufaika zaidi na
biashara ya kaboni nchini.
Hivyo, Waziri Nchemba ameliomba Bunge ridhaa ya kukusanya na kutumia jumla ya shilingi trilioni 56.49 kwa mwaka wa fedha 2025/26.