Featured Kitaifa

VRB YAWANOA WATHAMINI KUPITIA MAFUNZO YA UCHAMBUZI WA TAARIFA ZA KIFEDHA

Written by mzalendoeditor

 

Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wathamini FRV. Zidikheri Mndeme akifungua mafunzo ya uchambuzi wa taarifa za kifedha kwa wathamini tarehe 12 Juni 2025 katika Ukumbi wa PSSSFMillenium Towers, Jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya wathamini wakiwa katika mafunzo ya uchambuzi wa taarifa za kifedha kwa wathamini yalioandaliwa na Bodi ya Usajili wa Wathamini tarehe 12 Juni 2025 katika Ukumbi wa PSSSFMillenium Towers, Jijini Dar es Salaam.

Na. Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Bodi ya Usajili wa Wathamini (Valuers Registration Board – VRB) imefanikiwa kuandaa mafunzo ya siku mbili kwa wathamini, yaliyolenga kuongeza uelewa na umahiri katika uchambuzi wa taarifa za kifedha ‘‘Financial statements analysis for Valuers’’ kwa ajili ya uthamini wa kampuni au biashara mbalimbali.

Mwenyekiti wa Bodi hiyo FRV. Zidikheri Mndeme amefungua mafunzo hayo tarehe 12 Juni 2025 katika Ukumbi wa PSSSF, Millenium Towers, Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa ufunguzi huo, FRV.  Mndeme alieleza kuwa uelewa wa taarifa za kifedha ni msingi muhimu kwa wathamini katika kufanya uthamini wenye ufanisi, hasa katika mazingira ya sasa ya kiuchumi yanayobadilika kwa kasi.

‘‘Washiriki watajifunza mbinu za kisasa za kusoma, kuchambua na kutumia taarifa za kifedha katika kufanya uthamini wenye ufanisi’’ alisema Mndeme.

Kwa upande wao, washiriki walionyesha kuridhishwa na mafunzo hayo ambapo walikiri kuwa yatawasaidia katika kuongeza ufanisi utakao endana na mahitaji ya soko pamoja na kuongeza uaminifu katika taaluma hiyo.

Mafunzo haya ni sehemu ya juhudi za Bodi ya Usajili wa Wathamini kuhakikisha wathamini wanakuwa na ujuzi wa kisasa unaowawezesha kutoa huduma bora na zinazozingatia viwango vya Kimataifa.

About the author

mzalendoeditor