Featured Kitaifa

WAZIRI SIMBACHAWENE AITAKA TAKUKURU IKAZE UZI KWENYE RUSHWA NDOGO NDOGO

Written by mzalendoeditor

 

Na. Lusungu Helela – TABORA 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.George Simbachawene ameitaka Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) kuzidisha mapambano dhidi ya rushwa kubwa huku akisisitiza mapambano dhidi ya rushwa ndogo ndogo yasiachwe kwani ndizo zimekuwa kero kubwa kwa watu wengi hususan watu wa kipato cha chini katika maeneo ya  huduma za jamii nchini.

Amesema ni muda muafaka sasa kwa TAKUKURU kuanza  kushughulikia rushwa hizo ndogondogo  katika maeneo ya masoko, vituo vya polisi, shule, zahanati na maeneo mengine ya umma ambako baadhi ya watu wanajulikana na wamejigeuza bila kutoa chochote huwezi kuhudumiwa.

Mhe.Simbachawene ametoa kauli hiyo leo Mkoani Simiyu wakati akizindua jengo la Ofisi ya TAKUKURU Mkoa ambalo hadi kukamilika kwake limegharimu kiasi cha Sh.milioni 640.

Amesema rushwa za namna hiyo zimekuwa zikiwakera watu wengi wa tabaka la chini ambao ndio wengi hali inayochochea wananchi kuanza kuichukia Serikali.

Amesema wakishughulika na rushwa hizo wananchi watakuwa na furaha na watazidisha imani waliyokuwa nayo kwa Serikali yao.

Amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa mstari wa mbele katika vita dhidi ya rushwa, uwekezaji wake wa fedha, rasilimaliwatu na vitendea kazi ni utashi alionao kwa TAKUKURU ili iweze kufanya kazi yake kwa ufanisi.

” Rushwa ni adui wa ustawi wa jamii, rushwa inapofusha, TAKUKURU mpo kamateni vinara wa rushwa katika maeneo hayo kwani wanajulikana kwa majina na vyeo vyao  ” amesisitiza Mhe.Simbachawene. 

Kufuatia hatua hiyo, Mhe.Simbachawene ametoa wito kwa viongozi wa dini na wadau wengine kusaidia katika mapambano hayo kwani TAKUKURU pekee haiwezi na hivyo inahitaji ushiriki wa wadau  ili kukemea na kuwafichua wale wote ili sheria ichukue mkondo wake.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bw. Crispin Chalamila amesema Serikali imefanya uwekezaji mkubwa kwenye ujenzi wa majengo katika wilaya na mikoa mbalimbali nchini na hii ni kuonesha utashi wa Mhe.Rais katika mapambano dhidi ya rushwa nchini.

Amesema katika bajeti ya mwaka 2024/ 2025 kiasi cha shilingi Bilioni mbili zilitengwa kwa ajili ya   ujenzi wa majengo ya TAKUKURU nchini ikiwemo jengo hilo la TAKUKURU Mkoa wa Simiyu.

Chalamila amesema ujenzi wa jengo hilo utachagiza mapambano dhidi ya rushwa ambapo hapo mwanzo jengo walilokuwa wamepanga lilikuwa kwenye makazi ya watu hali iliyopelekea hata wale wananchi wenye taarifa fiche kuogopa kuja ofisini hapo kwa hofu ya kuonwa na watu, ” ila kwa ofisi hii  naamini wananchi watakuwa huru kutuletea taarifa bila hofu  ya kuonwa na yeyote ” amesisitiza Chalamila.

About the author

mzalendoeditor