TIMU ya Al-Hilal ya Saudi Arabia inataka kupeleka ofa Napoli kumsajili mshambuliaji Mnigeria anayetaka kuondoka, Victor Osimhen (26) kwa mshahara mnono wa Euro Milioni 40 kwa msimu na ongezeko la Euro Milioni 5 kulingana na kiwango chake.
Mpachika mabao huyo tegemeo wa Super Eagles anaheshimika kama mmoja wa washambuliaji mahiri kabisa duniani baada ya msimu mzuri uliomalizika akicheza Ligi Kuu ya Uturuki kwa mkopo katika klabu ya Galatasaray.
Osimhen amefunga jumla ya mabao 37 katika mechi 41 alizoichezea Galatasaray, ambayo imekuwa mchango mkubwa kwa klabu hiyo ya Istanbul kutwaa ubingwa wa ligi hiyo.
Galatasaray inataka kumbakisha Osimhen kwa mkopo wa Napoli na wameripotiwa kumpa ofa ya mshahara wa Euro Milioni 15 mshambuliaji huyo wa zamani wa Lille ya Ufaransa.
Osimhen mwenyewe ameripotiwa kwamba bado hajaamua juu ya mustakabali wake, kutonana na klabu nyingine pia ikiwemo Chelsea kuonyesha nia ya kutaka huduma zake.