Featured Michezo

RC SERUKAMBA AMSHUKURU RAIS SAMIA KWA KUIPA IRINGA UWENYEJI WA UMITASHUMTA NA UMISSETA 2025

Written by mzalendoeditor

OR-TAMISEMI

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Peter Serukamba, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuiamini na kuipa heshima Mkoa wa Iringa kuwa mwenyeji wa mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA kwa mwaka 2025.

Akizungumza leo, Juni 6, 2025, na waandishi wa habari mjini Iringa, RC Serukamba aliwahamasisha wananchi kuwapokea kwa moyo wa ukarimu wageni wanaoendelea kuwasili kushiriki mashindano hayo kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Visiwani.

“Hili ni tukio muhimu sana kwa Mkoa wa Iringa, kwa kuwa ni mara ya kwanza baada ya mashindano haya kufanyika kwa mfululizo mkoani Tabora hadi mwaka 2024. Tunamshukuru sana Mhe. Rais kwa heshima hii ya kipekee,” alisema RC Serukamba.

Aidha, alitoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kushuhudia ufunguzi rasmi wa mashindano hayo utakaofanyika tarehe 09 Juni 2025, ambapo mgeni rasmi atakuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (Mb).

Mashindano ya UMITASHUMTA yamepangwa kuanza rasmi tarehe 08 Juni 2025 hadi 17 Juni 2025, yakifuatiwa na UMISSETA yatakayodumu kuanzia 08 Juni hadi 30 Juni 2025.

Kwa mwaka huu, mashindano hayo yanatarajiwa kuvutia zaidi ya washiriki 10,000 wakiwemo wanafunzi, walimu wa michezo, maafisa pamoja na viongozi kutoka sekta mbalimbali za michezo nchini.

Michezo itakayoshindaniwa ni pamoja na mpira wa miguu, mpira wa kikapu, mpira wa wavu, mpira wa netiboli, mchezo wa kengele kwa wanafunzi wenye ulemavu wa kuona, pamoja na burudani ya muziki wa kizazi kipya.

Mashindano haya yatafanyika katika shule na viwanja mbalimbali ndani ya Mkoa wa Iringa, vikiwemo Shule ya Sekondari Wasichana Iringa, Shule ya Lugalo na Ualimu kleruu.   

About the author

mzalendoeditor