Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Mimba za utotoni, utoro mashuleni na kuvunjika kwa ndoto za elimu kwa watoto hasa wa kike vimeendelea kuwa mwiba kwa jamii ya Chemba mkoani Dodoma, vikichochewa na mila na desturi potofu zinazofundishwa kwa kisingizio cha kulinda utamaduni.
Katika kijiji cha Kidoka, baadhi ya ngoma za unyago na jando zimegeuka kuwa darasa la mapenzi kwa watoto ambao bado hawajakomaa kimwili wala kiakili, hali inayowasukuma kwenye hatari ya kupata ujauzito kabla ya wakati au kuachishwa masomo.
Kwa mujibu wa Sheikh Salamu Hando, mmoja wa wakazi wa kijiji hicho, anasema mafundisho yanayotolewa kwenye baadhi ya ngoma hizo yamepoteza mwelekeo wa asili na sasa yamekuwa chanzo cha kupotosha watoto.
“Tunawapa mafunzo ya ndoa na kuwashawishi kuwa ni watu wazima, jambo linalowachanganya na kuwaweka kwenye mazingira ya kuingia kwenye mapenzi mapema,” amesema.
Haayo yameelezwa hivi karibuni Wilayani Chemba,mkoa wa Dodoma katika mdahalo wa wazi ulioandaliwa na mradi wa Tuinuke kwa Pamoja kwa ufadhili wa Ubalozi wa Ireland, ukiwaleta pamoja wazee wa kimila, viongozi wa dini, wawakilishi wa serikali za vijiji, na mashirika ya kiraia ili kujadili namna ya kuondoa vikwazo vya kijinsia na kulinda haki za watoto.
Arafa Hukomo, mjumbe wa kituo cha taarifa na maarifa kijijini Kidoka, ameeleza kuwa kukosekana kwa sheria kali dhidi ya mila hizo kumeendelea kuwaingiza watoto wa kike katika hatari ya kupata ujauzito mapema na kuacha shule.
“Matokeo yake ni kukatizwa kwa safari yao ya elimu na kuathiri uwezo wao wa kujitegemea baadaye,” amesema.
Vijana wa kiume pia hawajasalimika Wengi wao hulazimika kuacha shule na kuelekea mijini kutafuta ajira zisizo rasmi, hali inayowatumbukiza katika maisha magumu na kuwaweka mbali na ndoto zao za baadaye.
Afisa Maendeleo ya Jamii wa kijiji hicho, Samalu Lupande, ameainisha kuwa umasikini wa kaya unachangia pakubwa matatizo haya.
“Wazazi huona elimu ni mzigo, hivyo huwashawishi watoto wasome kwa kiwango cha kawaida tu au waachane kabisa na shule ili wasaidie shughuli za kiuchumi nyumbani,”* amesema.
Lupande ameongeza kuwa hali hiyo huwafanya baadhi ya watoto wa kike kukubali msaada kutoka kwa watu wanaowalaghai kwa fedha au mahitaji ya shule kwa masharti ya ngono.
Amesema hali hiyo ni hatari kwa maendeleo ya jamii, kwani inaharibu kizazi na kuipa Serikali mzigo hapo baadaye ambapo watoto wanakuwa wameharibika nanmagonjwa au madawa ya kulevya.
Kwa upande wake, Vera Assenga kutoka Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), amesisitiza kuwa si kila mila ni potofu, bali ni muhimu kuchuja yale mafundisho yanayokinzana na haki na ustawi wa watoto.
Amesema ngoma za utamaduni zinaweza kubaki kama sanaa, lakini maudhui yake yafanyiwe marekebisho.
Amesema uwepo wa sheria rafiki kwa mtoto wa kike, utasaidaa kulinda maisha yao na kudumisha utamaduni wetu unaoendana na haki za kibinadamu.
Naye Deogratius Temba, Mwezeshaji wa mradi wa Tuinuke kwa Pamoja, amesema mijadala kama hiyo inalenga kuamsha jamii kijamii na kiakili ili kuchukua hatua za kubadili mwenendo wa mila na desturi zinazodhuru watoto.
Mdahalo huo umeibua mwamko mpya katika wilaya ya Chemba mwamko wa kuhoji, kuchuja, na kubadili mila zenye madhara kwa watoto.
Ni wazi sasa kuwa jamii hiyo inahitaji mabadiliko ya haraka, ili kuwapa watoto nafasi ya kutimiza ndoto zao bila vikwazo vya kimila.
Mwishoo