Featured Kitaifa

JAMII YAPASWA KUACHANA NA MILA POTOFU ZINAZOWABAGUA WATOTO WA KIKE

Written by mzalendo


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Amon Mpanju, akizungumza kwenye kikao cha tatu cha Kamati Tendaji ya Mpango wa Taifa wa Usawa wa Kijinsia kilichoandaliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kilichofanyika leo Mei 29, 2025 jijini Dodoma.

Mkuu wa Idara ya Uchumi na Utawala Bora katika Ujumbe wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Karina Dzialowska, akizungumza kwenye kikao cha tatu cha Kamati Tendaji ya Mpango wa Taifa wa Usawa wa Kijinsia kilichoandaliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kilichofanyika leo Mei 29, 2025 jijini Dodoma.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Amon Mpanju akisalimiana na Mkuu wa Idara ya Uchumi na Utawala Bora katika Ujumbe wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Karina Dzialowska, wakati wa kikao cha tatu cha Kamati Tendaji ya Mpango wa Taifa wa Usawa wa Kijinsia kilichoandaliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kilichofanyika leo Mei 29, 2025 jijini Dodoma.

Picha ya pamoja ya washiriki wa kikao cha tatu cha Kamati Tendaji ya Mpango wa Taifa wa Usawa wa Kijinsia kilichoandaliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kilichofanyika leo Mei 29, 2025 jijini Dodoma.

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Amon Mpanju, ametoa rai kwa jamii kubadilika na kuachana na mila potofu zinazowabagua watoto wa kike ili kuendana na mabadiliko yaliyo kwasasa ambapo wanawake wameanza kushika nyadhifa mbalimbali hasa Serikalini.

Naibu katibu Mkuu huyo ameyasema hayo leo Mei 29,2025 Jijini Dodoma wakati wa kikao cha tatu cha Kamati Tendaji ya Mpango wa Taifa wa Usawa wa Kijinsia kilichoandaliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chenye lengo la kuonesha mafanikio, changamoto na hatua zinazochukuliwa katika kuendeleza usawa wa kijinsia nchini.

“Nimefurahi kuwa kikao hiki muhimu kwani kinatupatia nafasi ya kujadili mafanikio na changamoto katika utekelezaji wa mpango huu. Tumegusia kwa kina sababu za kiwango cha chini cha utoaji taarifa za ukatili wa kijinsia, na namna tunavyoweza kuongeza ufanisi wa huduma za dawati la kijinsia mashuleni na katika jamii kwa ujumla”,amesema.

Aidha, Mpanju amebainisha kuwa kikao hicho kimetoa fursa ya kubuni njia za mabadiliko katika utoaji wa huduma za kijinsia, kujenga imani kwa wahanga, na kuimarisha mbinu za kuzuia na kukabiliana na ukatili wa kijinsia nchini.

Kwa upande wa Zanzibar, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Abeida Abdallah, amesema serikali ya Zanzibar kwa kushirikiana na UN Women na Umoja wa Ulaya imeendelea kutoa mafunzo na kujenga uwezo kwa watumishi wa umma na asasi za kiraia ili kuboresha huduma za kijinsia.

Naye, Mkuu wa Idara ya Uchumi na Utawala Bora katika Ujumbe wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Karina Dzialowska amesema wanajivunia kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika utekelezaji wa mpango huo wa mageuzi ya kijinsia.

“Tumetimiza miaka miwili ya utekelezaji, na kikao hiki kimetupa nafasi ya kuonyesha mafanikio, changamoto na mipango ya baadaye,”amesema.

Mpango huo unaoendeshwa kwa miaka saba umejikita katika maeneo muhimu kama vile kuongeza ushiriki wa wanawake katika uongozi, kuboresha upatikanaji wa mikopo na huduma za kifedha kwa wanawake, kupambana na ukeketaji na ndoa za utotoni kupitia mashirika ya kiraia kama Pastoral Women’s Council (PWC) na Kanisa la Kilutheri Tanzania (ELCT), pamoja na kusaidia wanawake na wasichana kupitia mfuko wa TASAF.

Umoja wa Ulaya umetenga Euro milioni 90 kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huu, ambapo Euro milioni 28 zinakwenda moja kwa moja katika bajeti ya Serikali ya Tanzania kwa ajili ya kuhakikisha masuala ya kijinsia yanazingatiwa katika mipango na bajeti zake.

Kikao hicho, ambacho ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa Mageuzi ya Usawa wa Kijinsia (Gender Transformative Action Programme 2021–2027) unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU), kimehusisha washiriki zaidi ya 65 kutoka serikalini, sekta binafsi, taasisi za kiraia, na wafadhili wa maendeleo.

About the author

mzalendo