WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Stergomena Tax, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya Wizara hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Mei 22,2025 jijini Dodoma
Na.Alex Sonna-DODOMA
KATIKA kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita,Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa,imefanikiwa kutatua migogoro ya ardhi iliyotambuliwa kwa kuhuisha mipaka, kupima maeneo, kufanya uthamini na kulipa fidia katika baadhi ya maeneo ya wananchi wanaostahili.
Hayo yameelezwa leo Mei 22,2025 jijini Dodoma na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Stergomena Tax,wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya Wizara hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Katika kipindi cha miaka minne kuanzia Mwaka wa Fedha 2020/21 hadi kufikia Februari 2025, wizara imefanikiwa kutatua migogogro ya ardhi 80 kwa kupima maeneo 263 na kuyapatia hati miliki maeneo 143. Aidha, wizara imefanikiwa kufanya tathmini na kulipa fidia jumla ya maeneo 61 yenye gharama ya Sh. 54,130,521,088.81,”amesema Waziri Dkt.Tax
Aidha ametaja mafaniko mengine katika sekta ya ulinzi kwa kipindi hicho cha miaka minne ni pamoja na ujenzi na ulinzi wa miradi mbalimbali ya kimkakati.
Dkt.Tax amesema kuwa miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa Ikulu ya Chamwino Dodoma, ulinzi wa Reli ya Kisasa (SGR), ulinzi wa mradi wa kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere, ulinzi wa mgodi wa Tanzanite uliopo Mirerani mkoani Manyara.
Pia, ulinzi katika bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutokea nchini Uganda hadi mkoani Tanga, ulinzi wa mradi wa kuchakata gesi asilia Likong’o mkoani Lindi na kivuko cha Busisi, ulinzi katika Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) hasa Bandari za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara, ulinzi wa Kampuni ya Simu (TTCL), ulinzi wa Viwanja vya Ndege na Uundaji wa meli katika Ziwa Victoria.
“Mafanikio hayo yamechangia katika kukuza uchumi na kuimarisha ulinzi, hususan katika maeneo ya kimkakati ambayo hayana budi kusimamiwa na Taasisi zitakazolinda maslahi ya Taifa. Hii imewezekana kutokana na uongozi mahiri wa Serikali ya Awamu ya sita,”amesema