Featured Kitaifa

KAMATI YA USHAURI USAJILI WA SARATANI YAZINDULIWA

Written by mzalendoeditor

Na WAF- Dodoma

Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Wizara ya Afya, Dkt. Caroline Damian amezindua Kamati ya Ushauri ya Usajili wa Saratani (ACCR) yenye lengo la kuimarisha Usajili wa Saratani nchini kupitia usajili unaozingatia idadi ya watu kwa kuwa na takwimu sahihi.

Uzinduzi wa Kamati ya Ushauri ya Usajili wa Saratani umefanyika leo Mei, 21,2025 Jijini Dodoma ambapo kamati hii inajumuisha wajumbe kutoka taasisi mbalimbali za Serikali, washirika wa kimataifa kama Vital Strategies, Mtandao wa Usajili wa Saratani Afrika (AFCRN), Shirika la Afya Duniani (WHO) na wawakilishi kutoka katika jamii, akiwemo manusura wa saratani.

Dkt. Caroline amesema kuwa Kamati Kuu itakutana mara mbili kwa mwaka, huku kamati ndogo tano zilizoko Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), Kituo cha Tiba Bugando, Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya, Kituo cha Tiba cha Kilimanjaro Christian Medical (KCMC), na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, zitakutana kila baada ya miezi mitatu.

“Takwimu sahihi ndiyo msingi wa mipango madhubuti ya sera, programu za kuzuia utambuzi wa mapema, matibabu bora na utunzaji kwa wagonjwa wa saratani,” amesema Dkt. Caroline.

Aidha, amesema kuwa kamati hiyo itakuwa bodi ya ushauri wa kitaalam kwa Wizara ya Afya, kwa lengo la kuimarisha Usajili wa Saratani nchini kupitia Usajili wa Saratani unaozingatia idadi ya watu.

Amesema kuwa hivi sasa, ni takriban asilimia 10.5 tu ya wakazi wa Kusini mwa Jangwa la Sahara wanashughulikiwa na sajili za saratani za idadi ya watu, nchini Tanzania, kukosekana kwa sajili ya kitaifa ya saratani inamaanisha kuwa takwimu za matukio ya saratani inayotegemea idadi ya watu haipatikani kwa ufasaha.

Dkt. Caroline ameongeza kuwa kamati hiyo ina majukumu makuu ya kutoa ushauri kuhusu mbinu bora za kukusanya takwimu za saratani, kuchambua mwelekeo wa matukio ya saratani na vifo, kutoa mapendekezo ya sera yenye msingi wa ushahidi, kusimamia utekelezaji wa mapendekezo yake na kuhakikisha kwamba takwimu zinapatikana kwa matumizi ya viongozi wa Serikali, watafiti na washirika wa maendeleo.

Vilevile amesema kuwa kwa mujibu wa Taasisi ya Global Cancer Observatory, Tanzania iliripoti takriban wagonjwa wapya 42,000 wa saratani na vifo 28,000 vilivyotokana na saratani mwaka 2020 makadirio yanaonesha kuwa matukio ya saratani katika maeneo yenye rasilimali ndogo barani Afrika, ikiwamo Tanzania, yataongezeka maradufu katika miongo miwili ijayo jambo linalosisitiza uharaka wa kuimarisha uchunguzi wetu na mifumo ya udhibiti wa saratani

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ufatiliaji na Tathimini kutoka Wizara ya Afya ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Bw. Claud John Kumalija amesema kuwa ndani ya siku mbili wanalenga kujadili na kutangaza kuundwa kwa Kamati ya Ushauri ya Tanzania ya Usajili wa Saratani kama hatua ya kimkakati ya kuimarisha usahihi na ukamilifu wa takwimu.

Ameeleza majukumu ya kamati ni pamoja na kusawazisha ukusanyaji wa takwimu, kuboresha mifumo ya kuripoti na kuongoza maamuzi ya sera, umuhimu wa usajili wa saratani na usaidizi kutoka kwa washirika, uwasilishaji wa ripoti ya Usajili wa Saratani ya Idadi ya Watu Tanzania, utayarishaji wa Mpango Kazi wa Mwaka wa kamati pamoja na kuweka wazi hatua za utekelezaji.

Vilevile, Bw. Kumalija amesema kuwa wanatarajia kamati hiyo kutoa mwongozo wa kimkakati wa usajili wa saratani, kuratibu juhudi za usajili za kitaifa na kikanda na kuhakikisha ujumuishaji wa takwimu za Usajili wa Saratani kwenye Mfumo wa Kitaifa wa Taarifa za Afya.

Bw. Kumalija ametoa rai kwa wadau na wajumbe wa kikao hicho kushirikiana kwa utalaamu ili kuwezesha kamati kusonga mbele kwa haraka kuelekea utekelezaji, ikiongozwa na mkakati wa kitaifa na dira ya kuhakikisha kwamba kila hatua wanayochukua inategemea takwimu sahihi na ya kuaminika.

About the author

mzalendoeditor