Featured Kitaifa

SERIKALI KUTATUA CHANGAMOTO YA KUFURIKA KWA MITO

Written by mzalendoeditor

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza akijibu maswali wakati wa Kikao cha 27 cha Mkutano 19 wa Bunge jijini Dodoma

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza akijibu maswali wakati wa Kikao cha 27 cha Mkutano 19 wa Bunge jijini Dodoma

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza akiteta jambo na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Omary Kipanga wakati wa Kikao cha 27 cha Mkutano 19 wa Bunge jijini Dodoma leo tarehe 19 Mei, 2025. Kulia ni Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Dunstan Kitandula.

…..

Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imesema inatarajia kuwezesha usafishaji na ujenzi wa kuta za mito yenye changamoto ya kufurika hasa wakati wa mvua ili kuwanusuru wananchi na kuathiriwa na mafuruko.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Khamis Hamza Khamis wakati akijibu maswali bungeni jijini Dodoma leo tarehe 19 Mei, 2025.

Akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kilombero Mhe. Abubakar Asenga aliyeuliza ni lini Serikali itafufua Mto Rumemo na kuboresha tuta la mto huo ili kupunguza athari za mafuriko katika Mji wa Ifakara mkoani Morogoro, Naibu Waziri Khamis amebainisha kuwa fedha zitakazotumika katika kazi hiyo zinatokana na bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais ya mwaka 2025/2026 ya zaidi ya shilingi bilioni 81 iliyopitishwa na Bunge hivi karibuni.

“Mheshimiwa Spika kupitia fedha za bajeti, kazi itafanyika ya kuondoa mchanga na kujenga kuta katika mito mbalimbali inayokabiliwa na changamoto ya mafuriko ikiwemo Kilombero, maeneo mengine ya Mtwara, Nungwi, Lindi na maeneo mengine hapa nchini,” alisema.

Awali akijibu swali la msingi la Mbunge wa Kondoa Mjini Mhe. Ally Juma Makoa aliyetaka kufahamu lini Serikali itaanza kazi ya kurejesha Mto Kondoa katika njia yake ya asili, Mhe. Khamis alisema Serikali kupitia Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) imefanya upembuzi yakinifu kwa lengo la kubaini chanzo cha kuhama kwa Mto Kondoa.

Naibu Waziri Khamis alitaja sababu zilizobainika kuwa ni pamoja na uwepo wa shughuli za kibinadamu zisizo endelevu kama vile ufugaji, kilimo, ujenzi na uchimbaji wa madini ndani ya mita 60 zinazosababisha kuongezeka kwa upana wa kingo za mto na kupungua kwa kina kutokana na kujaa kwa udongo ndani ya wa mto.

“Hali hii imesababisha wakati wa mvua maji kuacha njia yake ya asili na kuelekea kwenye maeneo mengine na kusababisha uharibifu wa mashamba na mmomonyoko wa udongo, hivyo ili kukabiliana na athari hizo, Serikali inaendelea kutoa elimu kwa umma na kuhamasisha jamii kuacha kufanya shughuli zisizo endelevu ndani ya mita 60 ya mto husika ili kupunguza tatizo la kuhama kwa mto huo mara kwa mara,” alisema.

Kutokana na changamoto hiyo, Naibu Waziri Khamis alitoa rai kwa wananchi kuendelea kuzingatia sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura 191 wanapofanya shughuli za kibinadamu ili kukabiliana na uharibifu wa Mazingira.

Katika hatua nyingine, Mhe. Khamis alisema zipo juhudi mbalimbali ambazo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais na Serikikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais zinashirikiana katika kutafuta fedha za kutekeleza miradi katika pande zote mbuli za Muungano.

Alisema hayo wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Amani Mhe. Abdul Yussuf Maalim aliyetaka kujua lini Serikali itapelekea fedha Zanzibar kukabili athari mabadiliko ya tabianchi.

Hivyo, Naibu Waziri Khamis alisema Serikali zote mbili zinashirikiana katika kushiriki mikutano ya kimataifa ambayo viongozi wanaitumia kuomba fedha za kutekeleza miradi Tanzania Bara na Zanzibar ikiwemo mabadiliko ya tabianchi, kupeleka mifugo, maji na ujenzi wa kuta.

About the author

mzalendoeditor