Featured Kitaifa

MAFUNZO YA WATAALAMU WA AFYA YA MIFUGO KIMATAIFA YAZINDULIWA

Written by mzalendoeditor

Na Mwandishi wetu

Serikali imezindua rasmi mradi wa mafunzo ya kimataifa kwa wataalamu wa afya ya mifugo, yanayofanyika katika nchi nne za Tanzania, Botswana, Zambia na Malawi.

Mafunzo hayo yameandaliwa kupitia mradi wa EDVET unaosimamiwa na Shirika la MIOUT, kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Hungary, Finland na Slovakia.

Akizungumza leo wakati wa uzinduzi wa mafunzo maalum kwa wataalamu hao jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na uvuvi, Prof. Riziki Shemdoe, amesema kuwa mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo vijana, hususan wahadhiri, ili waendane na mahitaji ya kisasa ya sekta ya ufugaji ndani na nje ya nchi.

Prof. Shemdoe ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeandaa Kampeni ya Kitaifa ya Chanjo dhidi ya magonjwa sugu 13 ya mifugo, kampeni ambayo inatarajiwa kuzinduliwa mwaka huu.

“Kampeni hiyo itaanza na magonjwa matatu, ambapo ng’ombe milioni 19, mbuzi na kondoo milioni 17, pamoja na kuku milioni 40 wanatarajiwa kuchanjwa kote nchini,” amesema Prof. Shemdoe.

Ameongeza kuwa kampeni hiyo itaambatana na mpango wa utambuzi wa mifugo kwa kutumia hereni, ili kurahisisha ufuatiliaji wa afya ya mifugo waliopatiwa chanjo pamoja na mahali walipo.

“Hii itamsaidia mfugaji kufuatilia afya ya mifugo wake na kufungua milango ya fursa katika masoko ya kimataifa,” amesisitiza Prof. Shemdoe.

Naye, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mafunzo ya Mifugo (LITA), Dkt. Pius Mwambene, amesema kuwa baadhi ya wahadhiri watapatiwa mafunzo ndani ya nchi, huku wengine wakipata fursa ya mafunzo ya juu katika nchi za Hungary, Slovakia na Ubelgiji, ili kuongeza ujuzi katika nyanja mbalimbali za afya ya mifugo.

About the author

mzalendoeditor