Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Katibu Mkuu Wizara Habari, Utamaduni, Sana na Michezo, Gerson Msigwa (kulia) kuhusu maboresho yaliyofanywa kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam alipokagua maandalizi ya Mashindano ya Michuano ya AFCON na CHAN yanayotarajiwa kufanyika nchini hivi karibuni. Kulia kwake ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Paramagamba Kabudi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
……….
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa leo Mei 17, 2025 amekagua ukarabati wa uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam ikiwa ni muendelezo wa ziara zake za kukagua maboresho ya viwanja kwa ajili ya maandalizi ya mashindano ya AFCON na CHAN yanayotarajiwa kufanyika nchini hivi karibuni.
Akiwa uwanjani hapo, Mheshimiwa Majaliwa ambaye aliambatana na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Profesa Palamagamba Kabudi pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Gerson Msigwa, amesema ameridhishwa na hatua za ukarabati zinazoendelea kiwanjani hapo.
Waziri Mkuu amesema kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na wakandarasi wanaokarabati uwanja huo ni kuwa upo tayari kwa michezo yoyote hata ya kimataifa na kwamba utakamilika kabla ya kuanza kwa mashindano ya CHAN na AFCON.
Aprili 7, 2025 Mheshimiwa Majaliwa alikagua ukarabati na ujenzi wa Viwanja vya Amani, Maisara na Mao Zedong Zanzibar, ambapo alisema Watanzania watapata fursa ya kuendeleza michezo na kuhamasisha wachezaji kufanya mazoezi zaidi ili wapate sifa za kucheza michuano hiyo. Kwa upande wa Tanzania Bara alikagua viwanja vya Shule ya Sheria, Gymkhan na Jenerali Isamuhyo.
Alisema uamuzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi wa kuridhia michuano hiyo kufanyika nchini utasaidia kwa kiasi kikubwa kuendeleza na kukuza sekta ya michezo na utalii nchini.
Aidha Mheshimiwa Majaliwa amesema ameridhishwa na kasi na bora wa ukarabati wa viwanja hivyo na jukumu lililopo kwa sasa ni kuilinda miundombinu hiyo ili ubora uliofikiwa baada ya ukarabati uendelee kuwepo hadi michuano hiyo itakapofanyika.