WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana, akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani yatafanyika katika Viwanja vya Chinangali Park, Jijini Dodoma kuanzia leo Mei 17 hadi 20 mwaka huu , yakibebwa na kaulimbiu “Nyuki kwa Uhai na Uchumi Imara, Tuwahifadhi.
Na.Alex Sonna_DODOMA
WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani itakayofanyika tarehe 20 Mei, 2025.
Hayo yameelezwa leo Mei 17,2025 na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana,wakati akizungumza na Waandishi wa Habari ambapo amesema kuwa maadhimisho ya mwaka huu yatafanyika katika Viwanja vya Chinangali Park, Jijini Dodoma kuanzia tarehe 17 hadi 20 Mei, 2025, yakibebwa na kaulimbiu “Nyuki kwa Uhai na Uchumi Imara, Tuwahifadhi.”
“Tanzania itaungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Nyuki Duniani itakayofanyika tarehe 20 Mei, 2025, kwa kuzingatia azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa la mwaka 2017, lililotangaza tarehe hiyo kuwa siku rasmi ya kuadhimisha mchango wa nyuki duniani.,”amesema Balozi Dkt. Chana
Na kuongeza “Kaulimbiu hiyo inaendana na maono ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan,”amesema Balozi Dkt. Chana
Waziri Dkt. Chana amesema maadhimisho hayo yanalenga kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa nyuki katika uchavushaji wa mazao, usalama wa chakula, na uhifadhi wa bioanuwai, huku akieleza kuwa tafiti zinaonesha asilimia 80 ya mazao ya chakula hutegemea uchavushaji unaofanywa na nyuki.
Akitoa ratiba ya Maadhimisho hayo Waziri Dkt. Chana amesema Tarehe 17 Mei 2025 utakuwa ni siku ya Ufunguzi rasmi wa maonyesho na matamasha ya nyuki mtaa kwa mtaa,tarehe 18 Mei 2025: Maonyesho yataendelea pamoja na semina kuhusu mnyororo wa thamani wa ufugaji wa nyuki.
Aidha ,tarehe 19 Mei 2025: Ziara za mafunzo kwa wadau katika viwanda vya mazao ya nyuki na tarehe 20 Mei 2025: Kilele cha maadhimisho kikiongozwa na Waziri Mkuu.
Amesema katika kipindi chote cha maonyesho, wananchi watakaotembelea viwanja vya Chinangali watapatiwa Tiba Nyuki bure, huduma inayojulikana kusaidia kuimarisha kinga ya mwili.
Aidha, kutakuwa na vivutio vya kipekee vya kitalii vikiwemo wanyamapori hai kama simba, tembo, ndege aina ya tausi na wengine wengi.
Waziri Dkt. Chana ametoa wito kwa Watanzania, hususan wakazi wa Jiji la Dodoma na mikoa ya jirani, kushiriki kikamilifu katika maadhimisho haya ya kimataifa yenye umuhimu mkubwa kwa taifa na dunia kwa ujumla.