Majid Abdulkarim, Dodoma
Hospitali Bingwa ya Taifa ya Magonjwa ya Akili ya Mirembe imehimiza umuhimu wa kufanya mazoezi ya mwili na kula mlo kamili kama njia ya msingi ya kulinda na kuimarisha afya ya akili.
Hayo yamesemwa Mei 17, 2025, na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Afya ya Akili kutoka hospitali hiyo, Dkt. Enock Chagarawe, wakati akizungumza wakati wa mwendelezo wa Kampeni ya Kitaifa ya Afya ya Akili inayoendelea jijini Dodoma inayolenga kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu ustawi wa afya ya akili.
Dkt. Chagarawe, amesema afya ya akili ni hali ya kuwa na utimamu wa kiakili na uwezo wa kushirikiana na watu wengine bila kujitenga.
Amebainisha kuwa matatizo ya afya ya akili huanza kwa mtu kuwa na msongo wa mawazo, hali ya kuwa na mawazo mazito au hofu bila kuwa na dalili za wazi za ugonjwa wa akili.
“Dalili nyingine ni pamoja na mtu kuamini kwamba amerogwa au kwamba watu wanamnyemelea kwa nia mbaya, kusikia sauti ambazo hazipo, kujitenga, kujiona hana thamani na hata kutamani kifo na wengne kuonesha tabia za hasira za mara kwa mara na kuwa wagomvi.”
Amefafanua kuwa watu wenye ugonjwa wa akili wanapaswa kupata matibabu ya kitaalamu katika hospitali na wakati mwingine kulazwa kwa ajili ya uchunguzi na tiba sahihi sambamba na huduma ya ushauri nasaha kutoka kwa wataalamu wa saikolojia pia ni muhimu katika mchakato wa matibabu.
Kampeni ya kitaifa ilianza
mkoani Dodoma, na tayari imeshatembelea mikoa ya Singida na Iringa, huku mikoa ya Morogoro na Manyara ikiwa katika ratiba inayofuata. Kaulimbiu ya kampeni inasema:
“Afya ya Akili ni Afya – Jikubali, Jijali.”
Kampeni hii ni sehemu ya jitihada za kitaifa za kubadili mtazamo wa jamii kuhusu afya ya akili na kuhamasisha watu kutafuta msaada mapema.