Featured Kitaifa

BODI YA NISHATI VIJIJINI (REB) YAPONGEZA MATUMIZI YA NISHATI SAFI GEREZA KUU LA ARUSHA

Written by mzalendoeditor

Wajumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB) wametoa pongezi nyingi kwa Uongozi wa Gereza Kuu la mkoa wa Arusha kwa kutoa kipaumbele kwenye matumizi ya teknolojia za Nishati Safi ya Kupikia wakati wa kuandaa chakula cha Wafungwa zaidi ya 700 tofauti na hapo awali ambapo matumizi ya kuni na mkaa yalikuwa makubwa kwa zaidi ya asilimia 100.

Akizungumza baada ya kutembelea Gereza Kuu la Arusha, tarehe 16 Mei, 2025 eneo la Kisongo nje kidogo ya Jiji la Arusha, Mhe. Balozi Radhia Msuya amesema Bodi ya Nishati Vijijini (REB); imeridhishwa kwa kiwango kikubwa na hatua zilizochukuliwa Gereza hilo katika kutekeleza agizo lililotolewa na Mheshimiwa, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alilolitoa mwezi Novemba, 2023 na kuzitaka Taasisi zote zinazowahudumia watu zaidi ya 100 kuacha kutumia nishati chafu (Kuni na mkaa) ili kupunguza matumizi ya kuni na mkaa ambayo yanachangia uharibifu wa mazingira.

“Tumekuja, kutembelea hapa Gereza Kuu la Arusha ili kujiridhisha; tumeona wanatumia kuni poa (Mkaa mbadala); Rafiki briquette pamoja na gesi ya kupikia majumbani (LPG). Jambo zuri kuhusu Mradi wa REA na Magereza ni kutoa fursa ya kuwezesha upatikanaji wa mashine za kutengeneza kuni poa na mkaa mbadala ambao unatokana na mabaki ya mazao mashambani, ambayo yanapatikana kwa urahisi kwenye Magereza mengi.” Amekaririwa, Mhe. Balozi, Radhia Msuya.

Baada ya kutembelea na kujionea miundombinu ya Nishati Safi ya Kupikia katika Gereza Kuu la Arusha; Wajumbe hao wa Bodi wamesema wameridhishwa kwa hatua zilizochukuliwa na Taasisi hiyo na kuongeza kuwa juhudi hizo, zitasaidia kufikia lengo la agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo Magereza Tanzania Bara itapata shilingi bilioni 35 kama ruzuku kutoka Serikalini kupitia REA ili kutekelezaji wa Miradi mbalimbali ya Nishati Safi ya Kupikia.

Kwa upande wake, Mkuu wa Gereza Kuu la Arusha, ACP, Charles Mihinga ameshukuru ushirikino uliopo baina yao na REA na kuongeza kuwa hapo awali hali ilikuwa siyo nzuri kwa kuwa chakula kiliandaliwa kwa muda mrefu pamoja na hali ya usalama wa afya za Waandaji wa chakula zilikuwa zikiathiriwa na moshi wa kuni pamoja na kiwango kikubwa cha nishati ya kuni kilikuwa kikitumika.

Kwa sasa tunatumia mkaa mbadala (Rafiki Briquettes); kuni poa zinapatikana hapa hapa Arusha pamoja na gesi ya kupikia majumbani (LPG) ambapo tumefungiwa mtungi mkubwa wa gesi wa tani 3.

Awali; Meneja Usaidizi wa Kiufundi kwa Waendelezaji Miradi, Mhandisi, Emanuel Yesaya kutoka REA amesema, REA ilisaini mkataba na Magereza ili kutoa ruzuku kwa ajili ya kuwezesha uboreshaji wa miundombinu ya Nishati Safi ya kupikia kwa Magereza yote Tanzania Bara.

“Mradi umelenga katika ujenzi wa miundombinu ya gesi asilia katika Gereza la Lilungu Mtwara, ujenzi wa miundombinu ya mitambo 126 ya biogas, ujenzi wa miundombinu 64 ya gesi ya LPG, usambazaji wa mitungi ya gesi 15,920 ya kilo 15 pamoja na majiko ya gesi ya ‘plate’ mbili kwa Watumishi wa Magereza, usambazaji wa mkaa mbadala (Rafiki briquettes) tani 850, ununuzi wa mashine 61 za kutengeneza mkaa mbadala pamoja na kuwajengea uwezo kwa Watumishi 280 wa Magereza kuhusu matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia”. Amekaririwa, Mhandisi, Yesaya.

About the author

mzalendoeditor