Na Mwandishi wetu, Dodoma
Benki ya Dunia (WB) yaihakikishia ushirikiano Serikali ya Tanzania kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) katika utekelezaji wa miradi ya Nishati kote nchini kwa ulinzi wa mazingira na ustawi wa Taifa kwa ujumla.
Hayo yamebainishwa Jijini Dodoma Mei 16, 2025 na Mtaalamu Mwandamizi wa Masuala ya Nishati Tanzania kutoka Benki ya Dunia, Dkt. Rhonda Antoine wakati wa kikao cha Ujumbe kutoka WB na REA kujadili hatua za utekelezwaji wa miradi ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, uendelezaji wa miradi ya nishati mbadala na mradi wa kusambaza umeme vitongojini kote nchini.
“Tunaipongeza REA; tunaahidi kuendeleza ushirikiano wetu kwa kazi kubwa inayofanya, tumeridhishwa na hatua mbalimbali zinazochukuliwa wakati wote wa kutekeleza miradi, vigezo vimezingatiwa,” alisema Dkt. Antoine
Akizungumza katika kikao hicho kilichokutanisha viongozi na wataalam kutoka REA na ujumbe huo wa Benki ya Dunia, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy alishukuru ushirikiano unaotolewa na benki hiyo katika kufanikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali inayosimamiwa na REA.
“Tunashirikiana kwa karibu na Wadau mbalimbali wa maendeleo ikiwemo WB katika kufanikisha utekelezaji wa miradi tunayoisimamia kwa mustakabali mzima wa maendeleo ya Watanzania wote,” alisema Mhandisi Saidy.
Alisema Serikali imeipa jukumu REA kutumia nyenzo na maarifa mbalimbali kuhakikisha umeme unafika kwenye vitongoji vyote nchini sambamba na kuhakikisha mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia unafanikiwa kwa kuhakikisha 80% ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Aliuhakikishia ujumbe huo kuwa REA itaendelea kusimamia vyema miradi iliyochini yake kama ambavyo miongozo mbalimbali ya WB inavyoelekeza.
Aidha, ujumbe huo wa WB uliipongeza REA kwa kuzingatia dhana ya usawa wa kijinsia wakati wote wa utekelezaji wa miradi pamoja na namna ambavyo inashirikiana na wadau kutoka Sekta Binafsi kutekeleza miradi.
Kikao hicho ni taratibu iliyowekwa na Benki ya Dunia kujadili hatua za utekelezaji wa miradi inayoifadhili na kufuatilia maendeleo ya utekelezwaji wake.