Featured Kitaifa

UCHUKUZI NA VIPAUMBELE VYAKE KATIKA BAJETI YA  2025-2026

Written by mzalendoeditor
Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa,akiwasilisha leo Mei 15,2025 bungeni jijini Dodoma  hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2025/2026.
Na.Alex Sonna-DODOMA
WIZARA ya Uchukuzi imetaja vipaumbele itakavyovitekeleza katika bajeti ya 2025-2026 ikiwemo kuendelea na ujenzi wa meli mpya na ukarabati wa meli zilizopo za kubeba abiria na mizigo katika Maziwa Makuu na Kuimarisha huduma za usafiri na usafirishaji majini.
Vipaumbele hivyo vimetajwa leo bungeni Mei 15,2025 na Waziri wa Wizara hiyo,Prof Makame Mbarawa wakati akiwasilisha bajeti ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2025-2026.
Waziri Mbarawa amesema katika mwaka wa fedha 2025/26, Wizara ya Uchukuzi itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia vipaumbele katika mwaka husika ili kuendelea kuimarisha utoaji wa huduma za uchukuzi nchini. 
Amevitaja vipaumbele hivyo ni Kuendelea na ujenzi wa Reli ya Kisasa ya SGR (Standard Gauge Railway) katika Ushoroba wa Kati; Kuendelea kuboresha miundombinu ya reli ya TRC (Metre Gauge Railway – MGR) na reli ya TAZARA – (Cape Gauge Railway – CGR) ikiwemo kipande cha kutoka Kilosa – Kidatu (km 108) kwa ajili ya kuunganishwa na reli ya TAZARA; Kuendelea kuboresha Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL).
Vipaumbele vingine ni  Kuendelea na ununuzi na ukarabati wa vitendea kazi ikiwa ni pamoja na vichwa vya treni, mabehewa na mitambo ya ukaguzi wa reli; Kuboresha miundombinu na 124 huduma katika Bandari za Bahari na Maziwa Makuu na kuendelea na ujenzi wa bandari kavu nchini, ikiwemo Bandari Kavu ya Kwala ambapo lengo ni kuifanya kuwa bandari kavu ya kimkakati.
Waziri Mbarawa ametaja vipaumbele vingine ni  Kuimarisha usalama na mawasiliano kwenye usafiri na usafirishaji katika Maziwa Makuu nchini; Uendelezaji na uendeshaji wa viwanja vya ndege; Kuimarisha usalama na udhibiti wa uchafuzi wa mazingira katika usafiri wa anga, ardhini na majini.
Vipaumbele vingine ni  Kuendelea na ujenzi wa meli mpya na ukarabati wa meli zilizopo za kubeba abiria na mizigo katika Maziwa Makuu na Kuimarisha huduma za usafiri na usafirishaji majini.

About the author

mzalendoeditor