…..
KATIKA mwaka wa fedha 2025-2026 Mradi wa uboreshaji wa Bandari ya Dar es salaam (DMGP) umetengewa jumla ya Sh bilioni 24.08.
Hayo yameelezwa leo Mei 15,2025 bungeni na Waziri wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi Prof Makame Mbarawa wakati akiwasilisha bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2025-2026.
Waziri Mbarawa amesema fedha hizo ni kwa ajili ya usimamizi wa utekelezaji wa mradi wa DMGP; ufungaji wa Mfumo wa Umeme katika Gati Na. 1- 7 pamoja na kufanya ukaguzi wa kitaalam wa mradi wa DMGP.
Pia amesema wametenga jumla ya Shilingi bilioni 13.80 fedha za ndani kwa ajili ya ukamilishaji wa Ujenzi wa Jengo la Abiria na Miundombinu na Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa Uboreshaji wa Kiwanja cha Mwanza.
Vilevile amesema wametenga fedha kwa ajili ya ukarabati wa uwanja wa ndege wa Kilimanjaro (KIA) jumla ya Shilingi bilioni 35 fedha za ndani kwa ajili ya kutekeleza kazi mbalimbali zikiwemo,ukarabati wa barabara ya kuruka na kutua ndege pamoja na mfumo wa taa za kuongozea ndege,ujenzi wa jengo la wageni mashuhuri, ujenzi wa uzio kuzunguka eneo la kiwanja; ujenzi wa Jengo la mizigo; na ujenzi wa jengo la utawala na watoa huduma.