Featured Kitaifa

BUNGE LAPITISHA BAJETI YA WIZARA YA UCHUKUZI TRILIONI 2.75 KWA MWAKA WA FEDHA 2025/26

Written by mzalendoeditor

 

Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa,akiwasilisha leo Mei 15,2025 bungeni jijini Dodoma  hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2025/2026.

…..

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kauli moja limeidhinisha Bajeti ya Wizara ya Uchukuzi yenye jumla ya Shilingi trilioni 2.746 kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu yake kwa mwaka wa fedha 2025/2026. Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 125.4 zimetengwa kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida huku Shilingi trilioni 2.621 zikitengwa kwa ajili ya utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo.

Akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo Bungeni, Waziri wa Uchukuzi Prof Makame Mbarawa ameeleza kuwa kati ya fedha za Matumizi ya Kawaida, Shilingi bilioni 96.7 ni kwa ajili ya mishahara ya watumishi na Shilingi bilioni 28.8 ni kwa matumizi mengineyo. Aidha, kati ya fedha za miradi ya maendeleo, Shilingi trilioni 2.45 ni fedha za ndani na Shilingi bilioni 168.5 ni fedha za nje.

Katika utekelezaji wa bajeti hiyo, Wizara itaendelea na miradi ya kielelezo kama ujenzi wa Reli ya Kisasa ya SGR na uboreshaji wa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), sambamba na miradi ya kimkakati kama uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam, ujenzi wa viwanja vya ndege mbalimbali nchini na uboreshaji wa usalama katika usafiri kwa njia ya maji na anga.

Serikali pia itaendelea na ujenzi wa meli nne za mizigo kwa ubia na sekta binafsi ili kuimarisha biashara kati ya Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kupitia Bandari ya Kigoma na Bandari ya Dar es Salaam ambapo Ujenzi wa meli hizo unatarajiwa kukamilika ndani ya miaka miwili.

Katika kuboresha huduma na miundombinu ya usafiri wa anga, ardhi na maji, Serikali itatekeleza miradi kama vile ujenzi wa Chuo cha Usafiri wa Anga, uimarishaji wa reli za MGR na TAZARA, pamoja na kuanzisha Kampasi ya NIT Lindi itakayotoa mafunzo katika sekta ya usafiri kwa njia ya maji, mafuta na gesi.

Hatua hii inaonesha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuimarisha sekta ya uchukuzi ili kuchochea ukuaji wa uchumi, kuongeza ajira na kuimarisha biashara ya ndani na nje ya nchi.

About the author

mzalendoeditor