Featured Kitaifa

WIZARA YA MAJI YAJIVUNIA DIRA ZA MAJI ZA MALIPO YA KABLA YA MATUMIZI

Written by mzalendoeditor
Waziri wa Maji Mhe.Jumaa Aweso akiwasilisha leo Mei 8,2025 bungeni jijini Dodoma makadirio ya Mapato ya Wizara hiyo kwa mwaka 2025-2026 .
Waziri wa Maji Mhe.Jumaa Aweso akiwasilisha leo Mei 8,2025 bungeni jijini Dodoma makadirio ya Mapato ya Wizara hiyo kwa mwaka 2025-2026 .
……
WIZARA ya maji imetaja mafanikio iliyopata ikiwemo kuanza kutumika kwa dira za maji za malipo ya kabla ya matumizi kwa wananchi na taasisi hivyo kuboresha huduma ya maji, kupunguza malalamiko ya wateja  kwenye ankara za maji.
Mafanikio hayo yametajwa leo Mei 8,2025 bungeni jijini Dodoma  na Waziri wa Maji Mhe.Jumaa Aweso wakati akiwasilisha makadirio ya Mapato ya Wizara hiyo kwa mwaka 2025-2026 ambapo ameliomba liidhinishe jumla ya Shilingi 1,016,894,958,000 kwa ajili ya matumizi ya Wizara ya Maji kwa mwaka 2025/26, ambapo Shilingi 73,779,579,000 ni za matumizi ya kawaida na Shilingi 943,115,379,000 ni za maendeleo.
Waziri Aweso ameyataja mafanikio mengine ni kukamilika kwa ujenzi wa mabwawa 45 madogo na ya ukubwa wa kati kwa ajili ya uvunaji wa maji ya  mvua ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya  tabianchi.
“Kuboreshwa kwa matumizi ya mifumo ya TEHAMA iliyowezesha uwazi na uwajibikaji katika makusanyo  na matumizi ya maduhuli yatokanayo na huduma za  maji.”amesema Mhe.Aweso
Vilevile amesema kuwa  Chuo cha Maji kuongeza udahili kutoka wanafunzi  2,320 hadi 4,260 sawa na ongezeko la asilimia 84.Kufanya tafiti na kutoa machapisho ya kisayansi 52.
Pia, kuanzisha Consultancy Bureau inayosaidia  kujenga uwezo kwa vijana wanaohitimu na Mfuko wa Taifa wa Maji kuendelea kuzijengea uwezo taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maji.
“Katika kuandaa maandiko ya miradi kwa lengo la kuongeza wigo wa  upatikanaji wa fedha ambapo kiasi cha Dola za Marekani Milioni 9.3 zimepatikana,”amesema Waziri Aweso

About the author

mzalendoeditor