WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima,akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 8,2025 jijini Dodoma kuelekea Siku ya Kimataifa ya Familia itakayofanyika Mei 15,mwaka huu.
…..
WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima,amesema Serikali imeendelea kuelimisha Wazazi au Walezi na jamii kwa ujumla kutimiza wajibu wao katika malezi na matunzo ya watoto na familia.
Waziri Gwajima ameyasema hayo leo Mei 8,2025 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea Siku ya Kimataifa ya Familia itakayofanyika Mei 15,mwaka huu.
“Nawahimiza Wazazi au Walezi kutimiza wajibu wao wa malezi na matunzo ya watoto kwa kuzingatia maeneo hayo muhimu ili kumkuza mtoto kuwa na tija kwa familia na taifa kwa ujumla.”amesema Dkt.Gwajima
Amesema katika kipindi cha Julai 2024 na Februari 2025, Wizara na Wadau wake kupitia Mwongozo wa Taifa wa Wajibu wa Wazazi na Walezi Katika Malezi na Matunzo ya Watoto na Familia imeendelea kutoa elimu ya malezi chanya kwa jamii kupitia vyombo vya habari, mikutano ya wazi na makongamano yanayohusisha wananchi na mitandao ya kijamii.
Aidha,amesema kupitia, wataalamu mbalimbali na viongozi wa dini wa ngazi ya Taifa walipatiwa mafunzo kuhusu malezi chanya ya watoto kutoka Jumuiko la Madhehebu ya Dini Matano ambayo ni Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Baraza la Waislam Tanzania (BAKWATA), Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Kanisa la Waadventista Wasabato (SDA) na Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT).
“Elimu ya malezi chanya iliwezesha kuendeleza elimu hiyo kwa waumini 3,800,000 kwa njia ya mihadhara na mahubiri katika nyumba za ibada pamoja na warsha na makongamano.”
Hata hivyo Waziri Gwajima ametoa wito kwa wataalamu na viongozi wa dini ni kuendelea kutoa elimu ya malezi chanya ya watoto na familia na kusisitiza mahusiano mema katika ndoa ili kuimarisha huduma za malezi ya watoto katika familia.
Amesema kuwa jitihada za kuimarisha malezi na matunzo ya watoto ikiwa pamoja na kuwaweka watoto na familia salama, Wizara imeendelea kuimarisha mifumo ya kisheria kwa kufanya marekebisho ya Sheria Tatu ambazo ni Sheria ya Mtoto, Sura ya 13, Sheria ya Makosa ya Kimtandao, Sura ya 443, na Sheria ya Msaada wa Kisheria, Sura ya 21.
“Marekebisho hayo yamelenga kuondoa upungufu unaojitokeza katika utekelezaji wa masharti katika sheria husika ili kuimarisha ulinzi na maslahi bora ya mtoto”amesema
Dkt.Gwajima ametoa rai kwa Wakuu wa Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa, Taasisi za Umma na Sekta Binafsi kuhamasisha na kuratibu matukio ya siku maalum za mtoko wa kifamilia katika maeneo yao, kwa kuzingatia mazingira na mila husika.