Na Mwandishi Wetu,Dodoma
Katika kukabiliana na changamoto za uendeshaji wa miundombinu ya michezo nchini, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imeanza mchakato wa kuanzisha chombo maalumu cha usimamizi wa miundombinu ya michezo nchini ambacho kitakuwa na mamlaka ya kusimamia uendeshaji, ukarabati na matunzo ya miundombinu yote ya michezo.
Hayo yamebainishwa leo Mei 7,2025 Bungeni Jijini Dodoma na Waziri wa Wizara hiyo Prof. Palamagamba Kabudi wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2025/26 ambapo ameliomba Bunge liidhinishe jumla ya shilingi Bilioni 519.6.
“Ni matumaini yetu kwamba kuwapo kwa chombo hiki kutapunguza changamoto za usimamizi wa miundombinu na kutaongeza thamani ya miundombinu ya michezo nchini,”amesema.
Aidha, ameongeza kuwa ili kuimarisha michezo katika ngazi za Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, Wizara hiyo imeratibu kikao kazi cha mwaka cha Maafisa Michezo Tanzania Bara.
“Kikao hiki kimefanyika sambamba na kikao kazi cha Maafisa Utamaduni nchini kuanzia tarehe 22-26 Aprili 2025 jijini Dar es Salaam, kikao kazi hiki kimejadili masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya michezo nchini yakiwamo utendaji kazi wa vitengo vya michezo na utamaduni katika ngazi za halmashauri nchini,”ameongeza.
Pia Prof. Kabudi amesema Serikali pia imeendelea na ujenzi wa viwanja vya mazoezi na kupumzikia wananchi ambao unatekelezwa katika Jiji la Dar es Salaam na Dodoma ambapo kwa upande wa Dar es Salaam mradi umefikia asilimia 46 na Dodoma mradi huu umefikia asilimia 65.
“Kukamilika kwa mradi huu kutatoa fursa kwa wananchi wa Dar es Salaam, Dodoma na Taifa kwa ujumla kuwa na viwanja vya kutosha vya mazoezi kwa ajili ya michezo mbalimbali ikiwamo, viwanja vya mpira wa mikono, viwanja vya mpira wa miguu, mpira wa wavu, netiboli, mpira wa kikapu, tenisi, na mchezo wa kuogelea.