Featured Kitaifa

WIZARA YA MADINI YAPANGA KUKUSANYA MADUHULI YA TRILIONI 1.4

Written by mzalendoeditor
Waziri wa Madini,Anthony Mavunde bungeni  wakati akiwasilisha hotuba ya  bajeti ya Wizara hiyo leo Mei 2,2025 bungeni jijini Dodoma kwa mwaka wa fedha 2025-2026.
…..
Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde ametaja  vipaumbele vya Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026, ambako imelenga kuimarisha mchango wa Sekta ya Madini katika kukuza uchumi wa taifa, kuongeza ajira, na kuinua ustawi wa jamii kupitia matumizi bora ya rasilimali za madini hapa nchini.
Ameyabainisha hayo leo Mei 02, 2025 Bungeni Jijini Dodoma wakati akiwasilisha Hotuba ya Mpango wa Mapato na Matumizi ya Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha wa Serikali wa 2025/2026 ambapo kupitia mpango huo, Wizara ya Madini imepanga kukusanya maduhuli ya shilingi 1,405,537,268,755.00 (Trilioni 1.4).
Ili kufikia lengo hilo la makusanyo ya maduhuli, Waziri Mavunde amebainisha kuwa, Wizara imeweka mkazo kwenye kuimarisha ukusanyaji wa maduhuli ya Serikali kwa kuhakikisha mifumo ya ukusanyaji mapato inaendelea kuwa ya kisasa, shirikishi sambamba na yenye uwazi. 
Waziri Mavunde amesema kuwa, hatua hiyo, inakwenda sambamba na lengo kuu la kuongeza mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa (GDP) hususan kupitia ongezeko la shughuli za uongezaji thamani na mauzo ya madini ndani na nje ya nchi. Itakumbukwa kuwa mchango wa Sekta kwenye GDP umefikia asilimia 10.1 mwaka 2024 ikiwa ni mwaka mmoja kabla ya muda ulioainishwa katika Sera ya Madini ya Mwaka 2009 na kwenye Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano 2021/2022 hadi 2025/2026. 
Aidha, Waziri Mavunde ameeleza kuwa, Vipaumbele hivyo pia vinaangazia kuendeleza mnyororo wa thamani kwenye madini muhimu na mkakati kama vile madini ya kielektroniki, ambayo yanatajwa kuwa nguzo ya maendeleo ya teknolojia duniani ambako kwa kufanya hivyo, Tanzania inalenga kujenga uchumi shindani unaotegemea maarifa na ubunifu.
Ameongeza kuwa, Wizara imedhamiria kuhamasisha uwekezaji katika Sekta ya Madini, huku kipaumbele kikiwa ni uongezaji thamani ndani ya nchi kabla ya kusafirishwa na kuuzwa nje ya nchi. Aidha, kuimarisha uendeshaji wa minada na maonesho ya madini ya vito ni hatua inayolenga kuongeza uwazi, ushindani, na thamani halisi ya madini yanayouzwa.
Sambamba na hilo, katika jitihada za kuhakikisha rasilimali za madini zinatumika kwa tija, Waziri Mavunde amesisitiza kuwa Serikali imepanga kuongeza uwekezaji kwenye tafiti za kina za madini, kwa kushirikiana na taasisi za kitaaluma na sekta binafsi, hatua itakayowezesha kugundua maeneo mapya ya uchimbaji, kuandaa ramani sahihi za kijiolojia pamoja na kuimarisha kanzidata ya jioliojia ya nchi.
Kwa kutambua mchango wa wachimbaji wadogo, Waziri Mavunde ameeleza kuwa, mpango huo umeweka kipaumbele cha kuwarasimisha na kuwaendeleza wachimbaji hao, kwa kuwapatia elimu, teknolojia, kuwaunganisha na taasisi za kifedha ili kupata mikopo yenye masharti nafuu kukuza mitaji yao na kuendelea kuwa masoko ya uhakika ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi, usalama na tija.
Pia, Waziri Mavunde amesisitiza kuwa, Serikali kupitia Wizara itaendelea kuzijengea uwezo taasisi zilizo chini ya Wizara ya Madini kama Tume ya Madini, Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini (GST) Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) pamoja na Taasisi ya Uhamasishaji na Uwazi katika rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia (TEITI) ili kusaidia kuboresha usimamizi, utafiti na uwekezaji katika sekta hiyo muhimu kwa maendeleo ya taifa.
Bajeti ya Wizara ya Madini kwa Mwaka 2025/2026 inalenga kujenga Sekta ya Madini imara, endelevu na shindani kimataifa kwa kuwa ni moja kati ya sekta inayozalisha ajira, kuongeza mapato ya serikali, na kuchochea maendeleo na miundombinu nchini, maendeleo ya kijamii na uchumi kwa ujumla.

About the author

mzalendoeditor